Harry Kane ajishtukia akiipigia hesabu Ballon d'OR
London, England. Straika wa England na Bayern Munich, Harry Kane anaendelea kufumania nyavu kwa kasi ya ajabu msimu huu, lakini ni kama amejishtukia baada ya kusema anatambua wazi matumaini ya kushinda Ballon d'Or yanategemea zaidi idadi ya makombe atakayotwaa msimu huu.
Nyota huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur iliyopo Ligi Kuu ya England (EPL), huyo mwenye umri wa miaka 32 anafurahia huenda msimu bora zaidi wa maisha yake ya soka akiwa na mabao 23 katika mechi 17 kwa Bayern, ambao haijapoteza mechi yoyote hadi sasa ikiongoza msimamo wa Bundesliga na pia katika kundi la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia amefunga mabao matatu katika mechi nne za England, yakiwemo mawili aliyoyapachika Oktoba wakati England iliilaza Latvia 5-0 na kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwakani.
Alipoulizwa kuhusu nafasi yake ya kuwania tuzo ya Ballon d'Or ya mchezaji bora duniani, Kane amewaambia waandishi wa habari juzi Jumamosi: “Naweza kufunga mabao 100 msimu huu, lakini nisiposhinda Ligi ya Mabingwa au Kombe la Dunia, huenda usishinde Ballon d'Or."
"Ni hivyo hivyo kwa (Erling) Haaland, ni hivyo kwa mchezaji yeyote. Lazima ushinde vile vikombe vikubwa,” ameongeza, akizungumza mchezo unaopigwa leo Jumapili wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Albania.
“Tuko katika hali nzuri sana Bayern Munich, jambo ambalo huenda likaniweka katika nafasi nzuri zaidi. Vivyo hivyo na England.
“Ikiwa mambo yataniendea vyema kwa klabu na nchi, basi bila shaka nitakuwa sehemu ya majadiliano ya kuwania tuzo kama Ballon d'Or.”
Ingawa England tayari imefuzu Kombe la Dunia, mechi zao za wiki hii dhidi ya Serbia na Albania ni sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea michuano hiyo.
Umuhimu wa michezo hiyo ulionyeshwa na uwepo wa beki Marc Guehi, ambaye licha ya kuumia, alijiunga na kambi na akahudhuria vikao vya timu kabla ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia uliopigwa Alhamisi.
“Kuwakilisha nchi yako ni heshima kubwa, na unapojaribu kujenga utamaduni na fikra ya ushindi, unahitaji wachezaji kuwepo kadiri inavyowezekana. Kila wakati ni muhimu,” Kane amesema Kane na kuongeza;
“Tunaendelea vizuri ndani na nje ya uwanja. Unaweza kuona kupitia kambi hii… Marc alipata jeraha dogo, lakini bado alitaka kuwa na kikosi, kuhudhuria mikutano na kujifunza tunachojaribu kufanya. Bila shaka naamini timu iko katika nafasi nzuri sana tunapoelekea mwaka ujao.”
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinatarajiwa kufanyika mwakani katika nchi za Marekani, Mexico na Canada, huku nchi 31 zimeshakata tiketi ya kushiriki, zikiwamo tisa za Afrika zikiongozwa na Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ghana, Tunisia, Morocco, Algeria, Cape Verde na Ivory Coast.