Hii ndiyo Qatar; Ina mafuta imenyimwa chakula

Muktasari:

  • Naam, watu wamezidi kuongezeka nchini Qatar na wingi huo unatokana na michuano mikubwa ya Kombe la Dunia inayokwenda kufanyika nchini humo.

Doha, Qatar. Naam, watu wamezidi kuongezeka nchini Qatar na wingi huo unatokana na michuano mikubwa ya Kombe la Dunia inayokwenda kufanyika nchini humo.

Lakini mbali ya rekodi na umaarufu wa michuano hiyo kuna mambo mengi ya kujua kuhusu Qatar yenyewe ambayo yatakufanya ufurahi na ushangae kwa wakati mmoja.


Baraka na mateso

Kwa mujibu wa tovuti mbali mbali Qatar ni miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani, ambapo utajiri wao unachangiwa zaidi na mafuta, gesi, mbolea na chuma.

Nchi nyingi kubwa duniani zinategemea biadhaa hizo na kwa kiasi kikubwa asilimia 17 ya gesi na mafuta ya nchini Japan yanatokea hapo, China((13.4%), Korea Kusini (15.6%), India (13.6%), huku nchi za jumuiya ya Ulaya asilimia 7.64 ya gesi na mafuta huwa zinatoka Qatar.

Lakini mbali ya kubalikiwa utajiri wa mafuta unaowaingiza pesa nyingi kila mwaka, Qatar ni nchi iliyonyimwa ardhi yenye rutuba na ndio maana imefungua viwanda vingi vya mbolea kwa ajili ya kuzitumia kupanda mazao mbali mbali.

Hata hivyo haijawasaidia kwani moja kati ya vitu ambayo imekuwa ikiagiza kwa wingi kutoka China, Marekani na nchi za umoja.


Hoteli kwa mwezi Sh8 milioni

Kwa mujibu wa tovuti ya Nomadlist, ikiwa unahitaji kutumia hotel za bei ghali zaidi unaweza kutumia kati ya Dola 8000 hadi 9000 za kimarekani kwa mwezi mmoja.

Lakini ikiwa bajeti ni ndogo unaweza kupata hoteli za kati chini ya dola 100 kwa usiuku mmoja ambapo zipo hadi hoteli za dola 85.

Bei hiyo huenda ikaongezeka zaidi katika kipindi hiki cha kombe la dunia ambapo watu wamezidi kuwa wengi na uhitaji umekuwa mkubwa zaidi.


Usafiri

Usafiri ni rahisi sana nchini humo, kwa ndani ya jiji la Doha, huwa inagharimu kati ya Riyal tatu hadi nne ambayo ni sawa na dola moja ya kimarekani, na usafiri kutoka jijini Doha kwenye miji mengine inagharimu kati ya Riyal nne hadi tisa.


Haya hutakifi kufanya Qatar

Wakati Afrika ya Mashariki na nchi nyingine duniani kuwa ni kawaida kumkumbatia au kumshika mkono mtu wa jinsi nyingine ni kawaida, kwa Qatari ni tofauti.

Hairuhusiwi kukumbatia, kugusana ama kumbusu mtu wa jinsi nyingine unapokuwa kwenye eneo la wazi ndani ya nchi hii na ukioneakana unaweza kupata adhabu ya kutozwa faini au kuondoshwa nchini na kufungiwa usitembelee tena.

Hata hivyo sheria inawaruhusu mke na mume na kugusana mikono ama mashavu lakini lazima wawe na uthibitisho wa cheti cha ndoa.

Kunywa pombe hadharani hairuhusiwi nchini Qatar na inaweza kumsababishia mhusika kufungwa ikiwa atakamatwa na mamlaka.

Hairuhisiw kutumia kidole kimoja kumuita mtu, aidha iwe mhudumu ama mtu mwingine yeyote, mbali ya kuita hata kuonyesha kitu kwa kidole kimoja pia nchini humo haitakiwi.

Lakini pia salamu ya kidole gumba ambayo imekuwa maarufu kwenye nchi nyingi duniani ikiwa ni ishara ya kukubaliana na kitu, nchini Qatar haitakiwi.

Kutumia kidole gumba kama salamu ama ishara ya kukubali jambo fulani inatafsiriwa kama moja ya tabia mbaya na inaweza kusababisha utozwe faini, ufukuzwe ama ufungwe.


Vyakula

Kuna vyakula vingi nchini humo lakini maarufu zaidi ambavyo pia vinapatikana maeneo mengi ni kama vile Waraq enab ambacho kimekuwa maarufu nchi nyingi za Kiarabu, vyakule vingine vinavyopatikana nchini humo ni-

Machboos: Ubwabwa ambao hutiwa viungo vingi na mchanganyiko vyama zaidi ya mbili ikiwa pamoja na nyama ya kuku, ngamia, kondoo na Ng’ombe.

Kousa Mahsi: aina ya maboga ambayo hupatikana zaidi China, Marekani na Hispania, lakini kwa Qatar upikwaji wake mara nyingi huwa ni kuchemshwa na kujazwa mchuzi wenye rangi nyekundu.

Saloona: Kitoweo kilichotengenezwa kwa mchuzi wa viungo mbali mbali na rundo la mboga za kienyeji

Karak chai: A strong tea.


Bila simu janja hutoboi

Kama ulikuwa umepanga kwenda nchini humo na simu ya kitochi, acha kuwa na mawazo hayo kwani kuna sheria mpya nchini humo inayohitaji kila mgeni kuwa na program maalumu iitwayo Ehteraz mobile app, kwenye simu yake.

Kazi ya program hiyo ni kufuatilia na kutunza hali na maendeleo ya virusi vya Corona na hali ya chanjo.

Ili kuinga kwenye maduka makubwa ama hotelini ni lazima uonyeshe program hiyo kwa walinzi waliopo mlangoni ndio uruhusiwe, tofauti na hapo hutopita.


Ijumaa inakuwa hivi

Ukiwa katika nchi hii ya kifahari siku ya ijumaa asubuhi hakuna shughuli yoyote inayoendelea zaidi watu kujiandaa na swala ya ijumaa.

Hakuna duka wala jengo lolote la kibiashara linalofunguliwa hadi saa saba au saa nane mchana ambapo watu watakuwa wameshamaliza kufanya ibada ya swala ya ijumaa.

Ukiamua kutoka na kutembea, utahisi kama unatembea kwenye eneo lililotelekezwa kwani hata watu pia muda huo huwa hawaonekani hadi swala itakapomalizika.


Si joto, baridi pia sana

Ni kweli kwamba ni moja kati ya nchi ambazo zina joto zaidi Duniani ni hii, kawaida kuna vipindi viwili, kipindi cha joto huanza Mei hadi Oktoba na baridi huanzia Desemba hadi February.

April, machi na Novemba ni miezi ambayo huwa haitabiriki, baadhi ya siku huwa na joto na siku nyingine huwa ni baridi.

Bila shaka katika kipindi cha michuano ya kombe la Dunia watu watakumbana na joto kali zaidi ambapo kwa sasa hadi kufikia hatua hiyo juzi joto inakadiriwa kufikia 49 hadi 50 kwa mchana na usiku hufikia 30 hadi 40.