Ishu ya majeraha ya Pacome, Aucho iko hivi

Muktasari:

  • Kwenye mchezo huo ambao vinara wa ligi Yanga walifungwa mabao 2-1, mastaa hao tegemeo walishindwa kumaliza mchezo kutokana na majeraha. Pacome aliumia katika dakika ya 28 na kutolewa ndani ya kipindi cha kwanza akiwa amebebwa akishindwa kutembea na kurudishwa vyumbani baadaye alionekana amefungwa bandeji kwenye goti.

Wakati mashabiki wa Yanga wakizidi kuwa na presha baada ya kuumia kwa wachezaji wao imefahamika ripoti ya wachezaji hao wawili walioumia kwenye mchezo dhidi ya Azam, kiungo Pacome Zouzoua na beki Yao Kouassi itajulikana ndani ya saa 72.

Kwenye mchezo huo ambao vinara wa ligi Yanga walifungwa mabao 2-1, mastaa hao tegemeo walishindwa kumaliza mchezo kutokana na majeraha. Pacome aliumia katika dakika ya 28 na kutolewa ndani ya kipindi cha kwanza akiwa amebebwa akishindwa kutembea na kurudishwa vyumbani baadaye alionekana amefungwa bandeji kwenye goti.

Yao naye aliumia mwishoni mwa kipindi cha pili na kutolewa akichechemea na kuongeza idadi ya majeruhi katika mchezo huo uliokuwa muhimu kwao.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema ripoti ya majeruhi hao wawili itatoka ndani ya saa 72 baada ya wachezaji hao kufanyiwa vipimo kujua ukubwa wa majeraha yao.

"Kweli wachezaji hao wamepata majeraha, madaktari wetu wanahangaika kupata majibu ya vipimo ambavyo wamefanya ripoti kamili tutaipata ndani ya masaa 72.

"Majeruhi tulionao sio wengi lakini wote ni wachezaji muhimu kwahiyo hata huku kwenye utawala tumekuwa tukipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakubwa kwa wadogo wa klabu hii wakitaka kujua hali zao

"Tuwaondoe hofu mashabiki na wanachama wa Yanga uongozi na madaktari, wanafuatilia kwa umakini mkubwa maendeleo ya wachezaji wao na tutawajulisha haraka," alisema Kamwe.

Mbali ya Pacome na Yao, Khalid Aucho pia ni majeruhi lakini ripoti zinasema Jumanne hii ataanza mazoezi mepesi. Yanga sasa inajiandaa na mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ikianzia Kwa Mkapa Machi 30.