Ishu ya Saido kutua Simba iko hivi...

SIMBA imeanza mipango ya kuimarisha kikosi chake kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa mwezi Desemba, mwaka huu huku supastaa Mrundi Said Ntibanzonkiza ‘Saido’ anayekipiga Geita Gold akitajwa kuwemo kwenye mapendekezo.

Simba inamfikiria Saido ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, viongozi wakiamini ataenda kuongeza nguvu kwenye eneo hilo ambalo kwa sasa linaonekana kucheza kwa kumtegemea zaidi Clatous Chama. Licha ya kwamba baadhi wanadai umri umemtupa Saido lakini wengi ndani ya uongozi wanaamini Saido atakuwa mbadala sahihi wa Chama kama atakuwa hayupo au kocha ataamua kumpumzisha lakini pia anaweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani kutokana na maamuzi ya kocha kwani tofauti na namba 10, staa huyo anaweza kucheza winga zote mbili, namba nane na hata mshambuliaji wa mwisho. Hii sio mara ya kwanza kwa Simba kutaka saini ya Saido kwani mwanzoni mwa msimu huu ilimfuata akiwa huru baada ya kutoka Yanga na kujadili ofa lakini mwisho wa siku ilishindwa kumsajili kutokana na sababu mbili.

Sababu ya kwanza ilikuwa ni mgawanyiko wa baadhi ya viongozi wa Simba ambapo wapo waliomhitaji Saido lakini wengine walisita kumsajili wakihofia ubora wake kushuka na badala yake wakaamua kumfuata Nelson Okwa nchini Nigeria ambaye hadi sasa hajaonyesha kiwango bora.

Kingine kilichokwamisha Saido kutua Simba ilikuwa ni kiasi kikubwa cha pesa alichohitaji na mabosi wa Simba kuona hastahili na kuamua kuachana naye lakini sasa wameamua kumrudia baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na Geita ambako ameshaanza kuaga.

Jambo lingine lililowafanya Simba kuitaka saini ya Saido mwenye mabao matatu na asisti nne hadi sasa ni uzoefu wake kwenye mechi za ligi na kimataifa wakiamini atawasaidia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huenda uhamisho huo ukakamilika kirahisi kwani chanzo cha ndani ya Geita Gold anakocheza Saido, kimelipenyezea Mwanaspoti kuwa staa huyo ni miongoni mwa wachezaji wasio na furaha kikosini hapo kutokana na ishu za masilahi na ameshawaambia viongozi kuwa Krisimasi anasepa.

Wengine wanaotajwa kung’oka Geita dirisha dogo ni Miraji Athuman ‘Sheva’, Kelvin Yondan, Ramadhan Chombo, Samson Sebusebu, Oscar Maasai, Hussein Bakari na George Mpole ambao kwenye siku za hivikaribuni kila mmoja amekuwa na ishu binafsi na uongozi.

Sambamba na Saido, Simba pia ina mpango wa kusajili mshambuliaji wa kati, kiungo wa kati na beki wa pembeni anayeweza kucheza kushoto na kulia ingawa bado wamekuwa wasiri sana kwa kuepuka kutibua mambo. Simba inataka kuingia na nguvu kubwa kwenye makundi ya Afrika lakini vilevile kuwa na wachezaji imara wa akiba kwenye benchi.