Chelsea, PSG ni fainali ya mkwanja mrefu

Muktasari:
- Tiketi za mechi hii zinaanzia dola 265 kwa baadhi ya tovuti zinazouza lakini pia kuna tiketi za bei ghali zaidi ambazo zinafikia dola 1,500.
New Jersey, Marekani. Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) imethibitisha ubora wake katika soka baada ya kuichapa Real Madrid mabao 4-0, sasa ikitarajiwa kuvaana na Chelsea kwenye mchezo wa fainali Jumapili ijayo, huku timu hizo zikikunja mabilioni ya fedha.
Chelsea ilifanikiwa kuitupa nje Fluminense kwenye mchezo wa nusu fainali juzi Jumanne, shukrani kwa mabao mawili yaliyofungwa na Joao Pedro ambaye anatarajiwa kufanya kazi kubwa kwenye mechi ya fainali.
Mchezo wa fainali utapigwa kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, Jumapili na tayari wachambuzi pamoja na mashabiki wanaipa nafasi kubwa PSG ya kutwaa ubingwa huo kutokana na kiwango ilichoonyesha kwenye michezo iliyopita kwenye michuano hii.
Ikiwa na mastaa wao Ousmane Dembélé, Fabian Ruiz na Gonçalo Ramos, vijana wa kocha Luis Enrique wametawala kwenye michuano hiyo huku wakipata ushindi kwenye mechi zote kubwa na endapo watatwaa ubingwa huu, watakuwa wameendeleza kile ambacho walifanya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo waliichapa Inter Milan mabao 5-0 kwenye mchezo wa fainali.
Kwa mujibu wa takwimu za fedha hadi sasa Chelsea imeshapata dola 88.43 milioni sawa na kitita ilichokunja PSG.
Kwa upande wa Fluminense iliondoka na dola 60.83 milioni na Real Madrid dola 59.43 milioni.
Hata hivyo, kwa upande wa Chelsea na PSG pesa walizopata zinaweza kuongeza kufikia kati ya dola 130 hadi dola 155 milioni ikitegemea na matokeo ya fainali.
Kiasi hicho cha dola 155 milioni ni mjumuisho ikiwa timu itashinda mechi zote za hatua ya makundi, pia ikashinda hatua zinazofuatia hadi fainali.

Vilevile ukiondoa pesa za ushindi kwenye mechi, dola 155 milioni ni mjumuisho wa pesa ambazo timu zimepewa kwa ushiriki wao ambapo timu za Ulaya ndio zinakunja pesa nyingi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa kila timu inayotoka Ulaya iliyocheza michuano hii imepata kati ya dola 12 milioni hadi dola 38 milioni ambazo zikiunganishwa na zile za ushindi, timu hujikuta zinapata kiasi hicho cha dola 130 milioni hadi dola 155 milioni.
Tiketi za mechi hii zinaanzia dola 265 kwa baadhi ya tovuti zinazouza lakini pia kuna tiketi za bei ghali zaidi ambazo zinafikia dola 1,500.
Kumekuwa pia na ulanguzi wa tiketi kwa watu wanaonunua kisha kuziuza kwa mashabiki wengine ambapo ripoti zinaeleza kuna watu wanauza tiketi hizo kwa zaidi ya dola 2000.
Hii itakuwa mara ya tisa kwa timu hizo kukutana kwenye michuano mbalimbali, huku mchezo huo ukiwa unatarajiwa kuwa mkali kwa pande zote.
Katika michezo hiyo iliyopita, Chelsea imefanikiwa kushinda michezo miwili, huku PSG ikishinda mitatu na mitatu na mingine ikimalizika kwa sare.
Zilianza kukutana Septemba 2004, PSG ikachapwa mabao 3-0, Novemba mwaka huohuo, mechi ilimalizika kwa suluhu Aprili 2014, PSG ikashinda 3-1, Aprili 2014, Chelsea 2-0 PSG, Februari 2015, PSG 1-1 Chelsea
Machi 2015, Chelsea 2-2 PSG, Februari 2016, PSG 2-1 Chelsea na Machi 2016, Chelsea 1-2 PSG.
Endapo kikosi cha kocha wa Chelsea, Enzo Maresca kitatwaa ubingwa huu itakuwa ni mara ya pili kwa klabu kutoka England kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Dunia mara mbili, huku PSG ikiwa haijawahi kutwaa ubingwa huo.
"Tunakwenda kwenye mchezo mkubwa wa michuano hii, hakuna wasiwasi wowote kuwa kila timu iliyofanikiwa kutinga fainali ni bora, tunakwenda kupambana kuhakikisha tunatwaa ubingwa," alisema Enrique.
Real Madrid ndiyo timu iliyotwaa ubingwa huo mara nyingi ikiwa imefanya hivyo mara tano ikifuatiwa na Barcelona mara tatu, Corinthias na Bayern Munich kila timu imetwaa ubingwa mara mbili.