Ivory Coast na ushindi wa kwanza Afrika Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Kombe la Dunia 2026 limeendelea kuwa na utam wake baada ya kushuhudia Ivory Coast ikipata ushindi wa kwanza huku Ujerumani ikitoa dozi nzito.
Ivory Coast imeandika historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kupata ushindi Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Ecuador 1-0 katika mchezo wa Kundi E.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na nyota wa Manchester United, Amad Diallo dakika ya 90 na kuipa timu yake pointi tatu muhimu katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo.
Ecuador walitengeneza zaidi nafasi nyingi kipindi cha kwanza baada ya kutengeneza nafasi kadhaa za wazi, huku mara mbili wakigonga mwamba. Hata hivyo, walishindwa kuzitumia nafasi hizo kabla ya kuadhibiwa mwishoni mwa mchezo.
Katika mchezo mwingine wa Kundi E, Ujerumani walitoa dozi nzito baada ya kuifunga Curaçao mabao 7-1.
Curaçao, wanaoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, waliwashangaza wengi kwa kupata bao la mapema kupitia Livano Comenencia, ambaye shuti lake lilimgonga kipa Manuel Neuer na kuingia wavuni.
Hata hivyo, Wajerumani walijibu kwa kasi na kuonyesha makali yao ya ushambuliaji kupitia mabao yaliyofungwa na Nico Schlotterbeck, Kai Havertz aliyefunga mawili, Jamal Musiala, Nathaniel Brown na Deniz Undav.
Katika Kundi F, Japan na Uholanzi ziligawana pointi baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Wakati huo huo, wawakilishi wengine wa Afrika Tunisia walipata pigo kufungwa mabao 5-1 na Sweden katika mchezo wao wa kwanza wa mashindano hayo.
Sweden walifungua ukurasa wa mabao mapema dakika ya saba kupitia Yasin Ayari, aliyenufaika na kosa la safu ya ulinzi ya Tunisia kufuatia mpira uliopigwa vibaya na kipa Mouhibb Shamach.
Bao hilo liliwapa nguvu Sweden ambao waliendelea kutawala mchezo na kuongeza mabao mengine kupitia Viktor Gyökeres, Alexander Isak na Mattias Svanberg.
Tunisia walipata bao lao pekee kupitia Rekik, lakini walishindwa kurejea mchezoni kutokana na makosa ya mara kwa mara ya safu yao ya ulinzi yaliyowapa Sweden nafasi zaidi za kushambulia.