Ivory Coast, Nigeria zatawala kikosi bora cha Afcon
Muktasari:
- Ivory Coast imetwaa ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika mwaka huu nchini humo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria kwenye fainali.
Dar es Salaam. Timu za taifa za Nigeria na Ivory Coast zimeteka kikosi bora cha fainali za Afcon mwaka huu baada ya kutoa idadi kubwa ya wachezaji wanaokiunda.
Miamba hiyo miwili ambayo ilikutana katika hatua ya fainali, kila moja imetoa wachezaji watatu katika kikosi hicho, kilichotangazwa leo Februari 24 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kana kwamba haitoshi, Ivory Coast pia imetoa kocha wa kikosi hicho ambaye ni Emerse Fae aliyeiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Mchezaji bora wa Afcon mwaka huu, William Troost Ekong ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Nigeria, waliotangazwa katika kikosi hicho, akiwa pamoja na winga Ademola Lookman na beki Ola Aina.
Kiungo mshambuliaji wa Ivory Coast, Franck Kessie pia amejumuishwa katika kikosi hicho pamoja na nyota wengine wawili wa Ivory Coast, beki Ghislain Konan na kiungo Jean Michael Seri.
Katika hali isiyotarajiwa, kikosi hicho hakina jina la mchezaji bora chipukizi wa mashindano hayo, Saimon Adingra wa Ivory Coast, ambaye anacheza nafasi ya winga.
Kama ilivyotarajiwa na wengi, kipa bora wa mashindano hayo, Ronwen William amejumuishwa kikosini.
Kwa mujibu wa CAF, wachezaji 11 wanaounda kikosi bora cha Afcon mwaka huu ni kipa Ronwen Williams (Afrika Kusini) na mabeki Ola Aina (Nigeria), Ghislain Konan (Ivory Coast), William Troost Ekong (Nigeria) na Chancel Mbemba (DR Congo)
Viungo ni Kessie na Seri wa Ivory Coast na mwingine ni Teboho Mokoena wa Afrika Kusini wakati washambuliaji ni Emilio Nsue (Guinea ya Ikweta), Yoane Wissa (DR Congo) na Ademola Lookman (Nigeria).