Mtibwa Sugar na dakika 1,080 bila ushindi ugenini, yafa tena Mbeya
Muktasari:
- Mbeya City imeshinda mchezo huo na kubaki nafasi ya 14 kwa pointi 25, huku Mtibwa Sugar ikiendeleza rekodi ya kutopata ushindi katika mechi za ugenini kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Mbeya. Mtibwa Sugar imeendeleza rekodi yake ya kutopata ushindi katika mechi zake za Ligi Kuu ugenini baada ya leo kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City ikiwa ni mchezo wake wa 12 bila kuonja pointi tatu.
Mchezaji Adil Buha ndiye aliibuka shujaa katika mchezo huo kufuatia bao lake la dakika ya 36 kwa mkwaju wa penalti na kuihakikishia pointi tatu Mbeya City na kuendeleza matumaini ya kukwepa kushuka daraja.
Hata hivyo licha ya ushindi huo, timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imebaki katika nafasi ya 14 kwa pointi 25 ikibakiza mechi nne kumaliza msimu huu na kusubiri hatma yake.
Baada ya mchezo huo, City itabaki nyumbani uwanja wa Sokoine kuwasubiri Simba, mchezo utakaochezwa Juni 17, saa 8 mchana ikihitaji ushindi ili kujinasua nafasi za chini na kuongeza matumaini ya kukwepa kushuka daraja.
Katika mchezo wa leo uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, timu zote zilionesha ubora na uwezo binafsi lakini wenyeji ndio walifaidika na dakika 90 kutokana na ushindi huo ambao umewaamsha upya katika kampeni ya kubaki salama Ligi Kuu.
Mtibwa Sugar licha ya kupoteza mchezo huo, lakini hawakuwa wanyonge kutokana na kumiliki mpira kwa asilimia kubwa japokuwa watajilaumu kwa nafasi walizopata bila kuzitumia na kukubali kulala kwa kichapo hicho.
Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu imefikisha mechi 12 ugenini bila kuonja ushindi ikiwa imepoteza mechi saba na kutoa sare michezo mitano na kuwa nafasi ya 11 kwa pointi 27 ikibakiza nne kuhitimisha msimu huu.
Akizungumzia matokeo ya leo, Kocha mkuu wa timu hiyo Yusuph Chipo amesema huenda haikuwa bahati yao kwa kuwa nyota wake walionesha kiwango bora lakini wakakosa kutumia nafasi walizopata kufunga mabao.
“Tunaenda kujipanga upya na tuwapongeze wapinzani waliopata bahati kushinda. Tunazo mechi nne za kupambania kubaki salama Ligi Kuu, vita ni ngumu lakini tunao uwezo wa kufanya tunachotarajia,” amesema Chipo.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Patrick Mwangata amewapongeza wachezaji kwa kujituma na kufanikisha ushindi akieleza kuwa matokeo hayo yameongeza kitu katika kukwepa kushuka daraja.
“Tunaenda kujipanga upya na mchezo ujao dhidi ya Simba, tunajua ugumu wake na umuhimu. Tutawaandaa vyema wachezaji kiakili na kisaikolojia kuhakikisha tunapata pointi tatu tuweze kujinasua mkiani,” amesema Kocha huyo.