Jesus atafutiwa mbadala Arsenal

Muktasari:
- Majina matatu yanatajwa kuwa mkononi mwa Arsenal na mojawapo kati ya nyota hao atatua klabuni hapo baada ya kufikia makubaliano ya kujiunga nayo.
London, England. Arsenal inaripotiwa imepanga kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika dirisha hili dogo la usajili ili kumnasa mshambuliaji ambaye ataziba pengo la Gabriel Jesus, aliyepata majeraha makubwa ya goti wiki iliyopita.
Siku mbili baada ya mchezo huo imeripotiwa kuwa atakosa mechi zote zilizobaki za Arsenal msimu huu na zile za mwanzoni mwa msimu ujao kwa vile atafanyiwa upasuaji mkubwa wa goti ili kutibu majeraha hayo.
Jesus amekutana na majeraha hayo katika kipindi ambacho Arsenal inamkosa nyota wake mwingine wa ushambuliaji, Bukayo Saka ambaye anauguza maumivu ya misuli na atarejea uwanjani mwezi Machi.
Na kutokana na hilo, Arsenal inatajwa kuwa ipo tayari kuvunja benki katika siku zilizobakia za dirisha dogo la usajili ili kumnasa mshambuliaji wa daraja la juu ambaye ataifanya iendeleze makali yake katika kipindi ambacho Jesus atakosekana.
Majina matatu yanatajwa kuwa mkononi mwa Arsenal na mojawapo kati ya nyota hao atatua klabuni hapo baada ya kufikia makubaliano ya kujiunga nayo.
Mshambuliaji anayepewa nafasi kubwa zaidi ni Dusan Vlahovic wa Juventus ambaye inaripotiwa kuwa ameshaiambia klabu yake kuwa hatoongeza mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo kwa vile anataka kutafuta changamoto mpya nje ya Italia.
Mwingine na mshambuliaji wa PSG, Randal Koro-Muan ambaye klabu yake ipo tayari kumtoa kwa mkopo katika dirisha hili la usajili na inaripotiwa ni miongoni mwa wachezaji ambao meneja wa Arsenal, Mikel Arteta anavutia kufanya nao kazi.
Changamoto ya Kolo-Muan inaonekana itakuwa ni sharti ambalo PSG wameliweka kuwa timu inayomtaka mshambuliaji huyo kwa mkopo hivi sasa, iwe tayari kumnunua moja kwa moja mwishoni mwa msimu kwa dau la Pauni 50.
Arsenal pia inatajwa kuvutiwa na nyota wa RB Leipzig, Benjamin Sesko ikiwa itashindwa kumnasa mmojawapo kati ya Vlahovic au Kolo-Muan.
Arteta alifichua mpango wao wa kusajili mshambuliaji ambaye ataongeza kitu kwenye timu yake.
"Tumepoteza wachezaji wawili wabunifu, enye umuhimu na wasiotabirika kwetu hivyo hilo lina athari kwa timu. Tuko kazini tukiangalia sokoni itakuwa ni ujinga kutofanya. Lakini hakuna mcheaji anayeweza kukuhakikishia anakuja leo na kuanza kufanya vizuri
"Tunatakiwa tuwe na tumaini, tuamini na tutajaribu kupata mtu. Tuko wazi sana juu ya wachezaji tunaowahitaji," alisema Arteta.