JICHO LA MWEWE: Fei Toto alivyotua CAS kwa kasi isiyohitajika

INACHOSHA lakini ndio hali halisi. Tunalazimika kumzungumzia Fei Toto, ingawa jana kulikuwa na mechi kubwa zaidi katika historia ya Tanzania iliyotazamiwa kucheza. Siwezi kumlaumu Fei. Haikuanzia kwake. Imeendelea kuwepo.

Soka la Tanzania lazima liwe na habari tofauti inayomhusu mtu mmoja ambayo inahamisha mwelekeo wote wa soka. Kabla ya Fei hapa majuzi tulikuwa na mgogoro wa Bernard Morrison. Zamani tuliwahi kuwa na migororo ya kina Ken Mkapa, Mohamed Mwameja, Ildefonce Amlima na wengineo ambao waliwahi kusaini timu mbili kwa wakati mmoja.

Na sasa mkononi tuna sakata la Fei. Tumeandikiwa katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii kwamba anataka kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhisi ya Masuala ya Michezo (CAS). Naam, tulijua tunaweza kwenda huko, kwa sababu upande wake wake umeonyesha nia ya kutokukutana na watu wa Yanga ili wamalize utata huu.

Kabla ya kila kitu, Fei ametuomba tumchangie mchango ili aweze kwenda CAS. Tumeshtuka kidogo kwa sababu Fei aliwahi kwenda katika benki moja katikati ya jiji akiwa tajiri na akaweka kiasi cha Shilingi 112 Milioni ili avunje mkataba wake na Yanga.
Imekuaje ghafla Fei hana pesa? Nadhani washauri wake pamoja na mtu aliye nyuma ya jambo hili ameshtuka. Kiasi ambacho awali Fei alipeleka benki kurudisha Yanga kilitengeneza imani kwa wengi kwamba kuna mtu amesimama nyuma ya jambo hili.

Fei alitoa wapi kiasi hiki? Analipwa Sh 4 Milioni kwa mwezi na Yanga. Hapo hapo ana matumizi yake mengi kama kijana ikiwemo kuitunza familia yake Zanzibar. Alitoa wapi kiasi hiki cha pesa? Kama TAKUKURU na TRA wangeenda mbali kuangalia kama alizochomoa pesa hizi katika akaunti yake au hapana, huenda angeingia katika matatizo.

Safari hii, aliye nyuma ya dili la Fei amejaribu kutumia akili ya kuonyesha kwamba hakuna aliye nyuma ya Fei katika biashara hii. Hata hivyo amechelewa. Watu wengi wameitumia kauli ya Fei ya kutaka achangiwe kama kebehi tu. Kwamba unamchangiaje mtu ambaye amekimbia mshahara wa Shilingi 4 milioni kwa mwezi? Watanzania wengi wanaota tu kupata mshahara kama huo.

Lakini lengo lilikuwa kusaidia kutengeneza huruma dhidi ya Fei. Sidhani kama imefanikiwa sana. Kinachoendelea ni kwamba watu wa Yanga wanatumia kutengeneza vikaragosi vya kebehi dhidi ya kauli hii. Wapinzani wao wanashindwa wafanye nini kwa sababu hiyo niliyoisema awali kwamba wanaona Fei alikuwa analipwa pesa nyingi kuliko kipato chao, hivyo hawaoni haja ya kumuonea huruma.

Na sasa Fei amekwenda CAS. Amekwenda kufanya nini? Kujaribu kuvunja mkataba wake na Yanga. CAS watawasikiliza Wanasheria wa Fei, pia watawasikiliza watu wa Yanga. Watu wa Yanga wataweka wazi kwamba Fei amepewa pia fursa ya kukutana nao na kuvunja mkataba.

Kuna mambo mengi ambayo yatawashangaza CAS, lakini mojawapo ni hili la Fei kugoma kwenda kukutana na watu wa Yanga kwa ajili ya kuvunja mkataba kwa amani. Yanga wamempa Fei njia tatu za kumaliza hili suala.

Kwanza ni kurudi klabuni na kuendelea kutumikia mkataba wake, pili ni kurudi klabuni kuangalia namna ya kuboreshewa mkataba wake, tatu ni kuangalia namna ya kuvunja wake sana sana kama kuna upande wa adui ambao umejificha na una dhamira ya kumchukua kutoka Yanga.

Fei hajaenda kuwasikiliza Yanga na hili ni jambo ambalo linatushangaza kidogo. Ninachofahamu Fei hana dhamira tena ya kucheza Yanga. Ninachofahamu Yanga hawana dhamira tena ya kuendelea kuwa na Fei. Kwanini wasikutane?
Labda kama wangekutana na Yanga wangehitaji pesa nyingi kutoka kwa Fei, huenda sasa kiungo huyo angekuwa katika nafasi nzuri ya kwenda CAS kwa sababu Yanga wangekuwa wanamkomoa. Sijui kama watu Fei na watu wake wanajua Yanga watahitaji kiasi gani kumruhusu yeye kuondoka.

Hatuwezi kujua majibu ya CAS yatakuaje kuhusu uhalali wa Fei kuondoka Yanga au vinginevyo. Kinachokera ni kwamba yote haya yanaendelea kuwa Fei akiwa hachezi tena soka. Kuanzia Desemba mwaka jana hadi leo hachezi tena soka.
Kuanzia hapo mpaka sasa amecheza mechi mbili tu za Taifa Stars. Ilikuwa dhidi ya Uganda pale Ismailia Misri halafu na lile la marudiano pale Temeke. Aliingia katika kipindi cha pili na hakuwa na madhara yoyote kwa sababu hakuwa fiti.

Walioanzisha hili sakata hawakujua kama litafika hadi mwezi huu. Keshokutwa ni Juni na Fei atakuwa anatimiza miezi sita bila ya kucheza soka la kishindani. Ujumbe wangu ulikuwa rahisi tu. Fei angeweza kuondoka Yanga bila ya hizi purukushani. Hazikuwa na maana yoyote.

Walio nyuma yake walidhani kwamba msimu wa soka ni mrefu au mkataba wa mchezaji ni mrefu. Alichopaswa kufanya Fei ni kuendelea kucheza Yanga bila ya kusaini mkataba mpya. Leo angekuwa amebakisha miezi takribani tisa tu ahamie timu ambayo anaitaka, tena akiwa na uhuru mkubwa kuliko hizi kasheshe za kuchangishana pesa pamoja na kutengeneza uhasama mkubwa na klabu iliyomkuza.

Wachezaji wengi mahiri siku hizi wanaondoka bure kwa sababu wanajua namna ya kutiririsha mikataba yao mpaka mwisho wa msimu. Msimu wa soka una miezi tisa tu na sio mwaka mmoja kama ambavyo wengi wanafikiria.

Kina Antonio Rudiger sio wajinga. Walikuwa wanajua hawatasaini mikataba mipya na walikuwa wanajua ni wapi watakwenda pindi mikataba ikifika mwisho. Maisha yangekuwa rahisi tu kama Fei angeamua kuchukua mkondo huu.
Tunavyozungumza ni kwamba hata maamuzi ya CAS hatujui yatakuja lini. Ni mchakato. Tuliona zile ‘nenda rudi’ katika sakata la Bernard Morrison. Huenda suala la Fei likafika hadi Desemba. Katika maisha yake ya mkataba halali ingekuwa ni suala la miezi mitano tu amalize mkataba wake.

Mpaka hapo hesabu ambazo zilipigwa na watu wake hazikufikiriwa. Fei angeendelea kucheza Yanga, hasa katika mechi hizi za kimataifa angekuwa anajiandaa vema zaidi kutua anakotaka kwenda akiwa wa moto. Yanga ingewasaidia tu kumuweka fiti mchezaji wao mtarajiwa. Zilikuwa hesabu ndogo ambazo waliosimama nyuma ya Fei hawakuweza kuzipiga. Ni kama vile walikuwa wanakimbizana na umri wa Fei wakati bado ni kijana mdogo.