JICHO LA MWEWE: Kwa Chama maandiko yametimia

Niliandika hapa wiki mbili zilizopita namna ambavyo uhusiano wa Clatous Chama na Simba unavyokaribia kukata roho. Hata ilipotangazwa wiki iliyopita kwamba Simba wamemsimamisha Chama sikushangazwa. Sasa hivi Chama na Simba wala hawapendani.

Unataka nimzungumzie Nassor Kapama kwamba naye amesimamishwa? Hapana. Hili jambo ni la Chama. Mchezaji tegemeo. Ni kama wakati fulani watani zao walimsimamisha Saido Ntibazonkiza halafu wakamsimamisha na Dickson Ambundo. Ukiisoma habari unaamini klabu inafanya kuwa sheria ni msumeno. Kumbe walaaa.

Hivyo, barua ya kusimamishwa kwa Chama haikunishtua. Wala yeye mwenyewe haikumshtua. Chama ameichoka Simba na Simba imemchoka Chama. Nilikuwa namtazama hapa majuzi akiwa amekaa katika benchi, huku nafasi yake ikichukuliwa na Willy Onana. Wala hakuonekana kujali zaidi ya kucheka na kupiga stori na washkaji wengine waliokuwa wamekaa katika benchi.

Sifa za mchezaji mahiri anayecheza mara kwa mara ni kwamba anachukia kukaa benchi. Anatamani kucheza. Anata-mani kuwepo uwanjani. Lugha yake ya mwili inapaswa kuonyesha amechukia. Kwa Chama ilikuwa hadithi tofauti. Alikuwa anacheka na kupiga soga katika benchi. Hakuonyesha kujali chochote kile kilichokuwa kinaendelea.

Na wakati hili likiendelea mashabiki wa Simba hawakuonyesha kukerwa na kitendo cha kocha Abdelhak Benchikha kumpiga benchi Chama. Kisa? Chama amewakera mashabiki wa Simba wa uwanja ndani na nje ya uwanja. Ni kwa muda mrefu sasa. Hajali sana uwanjani wala nje ya uwanja.

Nje ya uwanja mkataba wa Chama na Simba siku zote huwa unawaweka juu. Wakati fulani kabla hajaenda zake Mo-rocco ilikuwa inaonekana kama anaweza kwenda Yanga. Simba walikuwa wanasumbuka mno kuongeza mkataba wake na bahati mbaya katika mioyo ya mashabiki wa Simba sehemu ambayo ilikuwa inaonekana anaweza kwenda zake ni Yanga.

Na hata baada ya kurudi mashabiki wa Simba wamekuwa roho juu kuhusu Chama. Kumbuka mwanzoni mwa msimu ambavyo aligoma kwenda katika kambi ya mazoezi kule Uturuki. Simba walibaki roho juu. Bahati mbaya mashabiki wanakuwa hawajui mambo ya ndani kuhusu wachezaji wao na mikataba yao.

Na sasa nadhani hata mashabiki wamethibitisha kwamba kama wao wanavyomuhisi Chama basi ndio hali halisi inayowakumba viongozi. Hatimaye viongozi wameamua kuchukua uamuzi mgumu wa kumsimamisha. Ni uamuzi uliochukuliwa kwa roho nzito. Naamini hata pambano dhidi ya Wydad ambalo Chama alianza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki iliyopita viongozi na kocha waliamua kumpanga kwa moyo mzito.

Chama akafanya kile kile ambacho amekuwa akikifanya katika mechi kubwa miezi ya karibuni. Hakuonyesha utofauti wowote ambao zamani ulimfanya Chama kuwa Chama. Alicheza kivivu na kama kawaida yake katika siku za karibuni. Baadaye benchi likamuita huku akiwa hajafanya maajabu yoyote uwanjani. Zamani, unamtoaje Chama uwanjani katika mechi kama hii, huku Simba ikiwa inasaka matokeo na Chama akiwa hana majeraha?

Siku mbili baadaye Simba ikatangaza kumfungia kwa madai ya utovu wa nidhamu. Nazijua klabu zetu. Kama wewe ni mchezaji mahiri na hauna magomvi yoyote na klabu basi mara zote klabu inajaribu kukulinda hata kama umekosea kid-ogo au sana. Haitataka habari zipenye kwenda kwa vyombo vya habari wala mashabiki.

Hii Simba walijitokeza wenyewe na kwenda katika vyombo vya habari wakitangaza kumsimamisha Chama. Ulikuwa uamuzi mgumu kwa klabu, lakini umechelewa. Kwa muda mrefu Chama amewashika pabaya Simba kwa sababu ya uzembe wao wenyewe. Wamejitakia.

Ndio wamejitakia. Kwa muda mrefu sasa Simba wameshindwa kuondoa umuhimu wa Chama uliopitiliza klabuni. Wameshindwa kutumia madirisha mengi ya usajili kutengeneza kikosi imara ambacho kingeondoa kiburi cha wachezaji mahiri klabuni hapo. Upande wa pili wamefanikiwa katika hilo.

Kwa mfano, naamini Chama alikwenda katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya akaona wachezaji wengi waliosajiliwa ni wa kawaida. Akaamua kugoma kwenda Uturuki. Hakuona kama kungekuwa na mpambano mkubwa wa kutetea mshahara wake uwanjani.

Kwa muda mrefu Chama amewafanya Simba mateka kwa sababu anajua umuhimu wake uliopitiliza klabuni. Wakati yupo nchini, wakati amekwenda Morocco, na sasa amerudi, umuhimu wa Chama klabuni unaonekana kuwa mkubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote uwanjani. Aibu iliyoje.

Kule upande wa pili wamewahi kutokea wachezaji muhimu klabuni na wameondoka au kuondolewa lakini wao bado wapo katika mwendo mdundo. Ukweli unaouma ni kwamba Injinia Hersi Said hakosei sana kule kwa watani. Wameondoka Fei Toto na Fiston Mayele, lakini mwendo bado umebakia kuwa mdundo. Kwanini? Injinia hakukosea sana.

Ameondoka kocha Nasreddine Nabi lakini amekuja Miguel Gamondi ambaye kwa kiasi kikubwa ameliziba pengo la Mayele kwa timu kugawanya mabao mengi kwa viungo. Ameondoka Fei, lakini amekuja Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli. Wote wanafanya vizuri zaidi. Fei anafanya vizuri aliko, lakini huku alikokuacha kunafanya vizuri zaidi.

Hersi alipogundua kwamba Djuma Shaban anamsumbua akajua kwamba atampata Yao Kouassi. Hakuna kilichoharibika zaidi ya upande huo kufanya vizuri zaidi. Yannick Bangala alipoondolewa tayari nafasi yake ilijiziba kwa Mudathir Yaha-ya. Jaribu kufikiria kwamba wakati Mudathir akizurura Forodhani Zanzibar bila ya kazi Simba ilikwenda kumsajili Ismail Sawadogo.

Nafasi ya Chama angewekwa Pacome pamoja na Maxi labda Chama angeshika adabu. Sio hivyo tu, kuna wakati alipandisha sana kiwango chake kwa sababu nafasi ya ufalme wa Simba ilikuwa kama vile inakwenda kwa Jose Luis Mi-quissone. Unakumbuka nyakati zile?

Simba imeruhusu Chama awe mfalme kwa muda mrefu sana. Hili ni kosa kwa mchezaji wa Kiafrika. Kina Lionel Messi wanaweza kuendelea kuwa wapole hata kama wakiwa mastaa wakubwa lakini sisi Waafrika tuna matatizo makubwa pindi tunapopewa ustaa.