JICHO LA MWEWE: Labda huyu ndiye Aziz Ki waliyemtaka Yanga

TUENDELEE kusubiri kwanza. Msimu bado mrefu lakini labda huyu ndiye Aziz KI waliyemtaka Yanga. Aziz KI wa msimu huu na sio yule wa msimu uliopita ambaye alikuwa bingwa wa matukio. Alikuwa anawapiga Yanga matukio kisha anakaa kimya tu.

Alifunga bao muhimu la kusawazisha dhdi ya watani halafu akafunga bao muhimu dhidi ya Club Africain pale Tunisia. Hata hivyo, muda mwingi alikuwa akiwakera Yanga na kocha wao, Nasireddine Nabi. Aziz asiyekaba, Aziz anayepoteza mipira. Aziz mzito.

Kichekesho kikubwa ni matarajio ya watu wa Yanga ambao waliamini kwamba Aziz Ki ndiye angekuwa jibu lao kwa kiungo wa Simba, Clatous Chotta Chama ambaye ametamba kwa muda mrefu katika soka letu katika eneo la kiungo cha ushambuliaji. Vilikuwa vitu viwili tofauti.

Hata yeye mwenyewe tukiwa hotelini Tunisia aliwahi kunifuata na kuniambia anashangaa namna ambavyo vyombo vya habari vimekuwa vikijaribu kumlinganisha na Chama huku akiamini Chama alikuwa mkali zaidi yake. Na kwa sababu hiyo ndiye mchezaji pekee wa Simba ambaye anayemfuatilia katika mtandao wa Instagram.

Mwishoni mwa msimu Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said aliamua kuchukua maamuzi magumu kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu. Akamtema Djuma Shaban. Akamtema Yannick Bangala. Akamuita ofisini Aziz KI na kutaka kuchana mkataba wake uliobakiza mwaka mmoja. Aziz akaahidi kupambana. Ilikuwa aondolewe.

Mashabiki wa Yanga wasingelia. Wasingemnunia Hersi kwa sababu hata wao walikuwa hawamwelewi Aziz. Walimjua Aziz halisi ambaye walikesha usiku wa manane kusubiri atambulishwe mitandaoni akitokea ASEC Mimosas. Huyu waliyekuwa wanamshuhudia alikuwa feki.

Labda sasa anajibu mapigo. Tayari ana mabao saba katika michuano mbalimbali msimu huu. Msimu bado mchanga sana. Jumatatu usiku aliondoka na mpira wake katika pambano dhidi ya Azam FC. Katika vyumba vya kubadilishia nguo akampa mpira huo, Anthony Mavunde, waziri wa madini kama zawadi.

Sio tu kwamba amefunga mabao mengi lakini pia amecheza vizuri katika mechi zote alizopangwa. Ameacha ubinafsi, amekuwa mwepesi, anacheza kitimu, anatumia maarifa binafsi. Anafunga na anatengeneza mabao kwa wenzake. Kumbuka pasi yake kwa Clement Mzize pale Kigali katika pambano dhidi ya El Marreikh.

Huyu ndiye Aziz ambaye Yanga walikuwa wanamtaka? Inawezekana. Kwanza anacheza katika presha kubwa ya kupata mkataba mpya. Ni msimu wake wa mwisho na katika msimu uliopita soko lake lilishuka. Hakuna ambaye angemtaka. Hata Mashujaa wa Kigoma wasingemtaka. Aliishi kwa matukio machache tu halafu basi.

Msimu huu inaonekana anasaka mkataba. Lakini hapo hapo amegundua kwamba Yanga hawaaminiki. Wana roho ngumu. Hawaangalii sana namna ulivyokuja kwa mbwembwe. Kumbe wanaweza kukubali hasara na kusonga mbele. Ungeweza kudhani Yanga ingeachana na Bangala hasa baada ya kiwango alichoonyesha katika msimu wa kwanza?

Ungeweza kudhani Yanga ingeachana na Djuma baada ya kelele zote zile za uhamisho wake akiwa mmoja kati ya mabeki bora wa kulia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa akiwa na AS VITA? Nadhani Aziz amehisi kwamba kumbe yote haya yanawezekana. Labda ndio maana amepania usiku huu. Zile mbwembwe zote za kutambulishwa usiku zinaweza kuwa bure tu katika soka letu.

Lakini naambiwa kwamba ujio wa Max Nzingeli na Pacoume Zouazou umemuamsha. Wote wamemwambia kocha wao kwamba wanajisikia raha na amani zaidi wakicheza katika nafasi ya Aziz KI. Bahati tu kwa Aziz kwamba Kocha Miguel Gamondi anamudu kuwachezesha wote watatu kwa ufasaha.

Kama angekuwa hawezi kuwachezesha wote kwa ufasaha inamaanisha kwamba kwa kiwango alichoonyesha Aziz msimu uliopita basi angepigwa benchi na wageni hawa ambao ni bora kuliko Aziz kwa msimu uliopita. Safari hii amekwenda nao sambamba.

Lakini kuibuka kwa Aziz labda pia kunatokana na mabadiliko ya kocha. Aziz hakuwa vizuri na Nabi. Inaonekana Gamondi anajua kumtumia Aziz katika mfumo wa kucheza huru ‘free role’. Lakini pia inawezekana Gamondi amemuwekea mkono begani na kumfanya kuwa kama ‘last born’ wake. Kwamba anampenda na anamtumainia.

Wakati mwingine wachezaji wanahitaji kuaminiwa na kocha. Ghafla wanajisikia kucheza soka tena kwa mara ya mwisho. Huwa inatokea wakati mwingine kutokana na malezi tofauti ya wachezaji wetu. Nao ni binadamu. Naambiwa Aziz ni ‘mtoto wa mama’. Labda kuna namna tofauti anayojisikia akicheza chini ya Gamondi tofauti na ilivyokuwa kwa Nabi.

Lakini pia inawezekana kilichombadilisha Aziz msimu huu ni mazoea na nchi yenyewe. Achilia mbali mambo mengine ya kawaida lakini si ajabu amejua deni kubwa linalomkabili mchezaji wa Yanga au Simba pindi anapoingia uwanjani. Deni hili huwa haliwakabili wachezaji wa Azam FC wala wa klabu nyingine yoyote nje ya Simba na Yanga. Labda amejua thamani hii.

Tuhifadhi maneno msimu bado mchanga lakini labda huyu ndiye Aziz ambaye walimfuata Abidjan kuja kucheza Yanga. Labda. Kama kweli amejitafuta na amejipata basi huenda Yanga akawa kama usajili mpya ndani ya Yanga. Huenda akawafuta machozi watu wa Yanga.

Kuna kawaida kwa klabu hizi kupata hasara ambazo hazisemwi. Wachezaji wanakuja kwa mbwembwe kubwa huku klabu zikitumia pesa nyingi lakini mwisho wa siku hakuna cha maana wanachofanya zaidi ya kwenda Beach Kidimbwi kustarehe wakati kina Dickson Job, Mohammed Hussein Tshabalala, Shomari Kapombe, Bakari Mwamunyeto, Aishi Manula na wengineo wa hapa nyumbani wakichapa kazi.

Kama Aziz angerudi tena katika msimu huu kama ilivyokuwa msimu wa kwanza basi kifupi tu Yanga ingekuwa imepata hasara kwa nyota huyu wa Burkina Faso ambaye ni mmoja kati ya nyota wanaolipwa pesa nyingi nchini. Kama akiendelea hivi hivi basi Yanga itakuwa haijapata hasara.

Hawa kina Mamadou Doumbia,  Djuma Shaban, Peter Banda, Osumane Sakho na wengineo wametupiga tu hasara za kimya kimya ambazo hatutaki kukubali. Aziz alikuwa anaelekea huku mpaka alipobadilika msimu huu. Akiendelea hivi hivi huenda tusiseme kwamba Yanga wamepata hasara.