Juventus yajitosa kwa Tonali
Klabu ya Juventus ina mpango wa kumvuta kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali, na inadaiwa wako tayari kumtoa mshambuliaji wao Dusan Vlahovic kama sehemu ya dili hilo.
Kwa mujibu wa Gazzetta dello Sport, Juventus wanamwona Tonali kama mchezaji wa ndoto, hasa baada ya kuonyesha kiwango kizuri msimu uliopita akiwa na Newcastle, licha ya kutumikia adhabu ya miezi 10 kwa kukiuka sheria za michezo ya kubashiri. Mchezaji huyo mwenye miaka 25 alicheza mechi 45, akisaidia klabu hiyo kushinda Kombe la Ligi na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ingawa wanajua si rahisi kumsajili, Juventus wanatarajia kutumia hali ya sintofahamu iliyopo Newcastle, ikiwemo tetesi za Alexander Isak kutaka kujiunga na Liverpool.
Katika ofa yao, Juventus wako tayari kumtoa Vlahovic, ambaye amebakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake na analipwa pauni 321,000 kwa wiki. Aidha, wanaweza kuongeza majina mengine kama Douglas Luiz au Nicolo Savona, pamoja na pesa, kwa kuwa wanatambua thamani ya Tonali ni kubwa zaidi.
Kwa upande wa Newcastle, msimu huu wa usajili umekuwa mgumu baada ya kukataliwa na wachezaji kadhaa akiwemo Benjamin Sesko aliyejiunga na Manchester United, Bryan Mbeumo, Joao Pedro, Matheus Cunha, Marc Guehi, na James Trafford.
Hata hivyo, bado wana matumaini kwamba dili la Yoane Wissa kutoka Brentford litakamilika mara tu klabu hiyo ya London itakapopata mbadala wake.