Kagera Sugar FC wababe U-20, waichapa Azam FC

Dar es Salaam. Ligi ya Vijana chini ya miaka 20 (U20 Youth League) imemalizika na tayari bingwa wa michuano hiyo Kagera Sugar FC yenye maskani yake mkoani Kagera baada ya timu hiyo kuibuka bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2023/2024 kufuatia ushindi wake wa penati 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji FC (U20).

Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika  jana katika uwanja wa Chamazi Complex  jijini Dar es Salaam ikihusisha  ushindani mkubwa baina ya timu hizo mbili hali iliyosababisha hadi dakika 90 zinakamilika matokeo yakiwa 0-0 na hata zilipoongezwa dakika nyingine 30 bado matokeo yalibakia kuwa hivyo hivyo na hatimaye mshindi kuamuliwa kwa njia penati.

Mkurugenzi wa Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC ambao ni wadhamini, Peter Nalitolela aliiwakilisha benki hiyo kwenye tukio hilo lililopambwa na uwepo wa mashabiki na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Nalitolela alisema tukio hilo limehitimisha utoaji vikombe vya ligi zote tatu zinazodhaminiwa na benki hiyo kwa msimu 2023/2024 kuanzia kwa kukabidhi kikombe cha cha Ligi ya Championship kwa timu ya Kengold ya mkoani Mbeya mapema mwezi huu huku makabidhiano ya kikombe kingine yakiwa ni yale yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo ilishuhudiwa benki hiyo ikitumia helkopta kuleta kikombe cha Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi kwa mabingwa wa ligi hiyo timu ya Yanga SC yenye maskani yake mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.

“Kimsingi tunawapongeza sana vijana wa Kagera Sugar (U20) kwa mafanikio haya na hivyo wanaungana na mabingwa wengine wawili ambao tayari wamefamikiwa kutwaa vikombe hivi kwa msimu wa 2023/2024. Msukumo wa kudhamini ligi hii ya vijana unachagizwa na dhamira yetu ya kuwa na ligi kuu yenye ubora na ushindani kutokana na vipaji vinavyozalishwa hapa nchini.’’

“Umuhimu wa uzalishaji wa vipaji hivi unaonekana pia hata kwenye timu ya taifa. Hivyo huu ni mwanzo tu tutaendelea kuboresha zaidi udhamini wetu ili kupata matunda mazuri zaidi,’’ alisema Nalitolela

Zaidi Nalitolela alibainisha kuwa kukamilika kwa ligi hizi kunatoa fursa kwa benki hiyo kuendeleza programu nyingine za michezo ikiwemo kiliniki yake ya vipaji kwa watoto wadogo yaani NBC Football Kliniki sambamba na  maandalizi ya mbio za Dodoma Marathon zinazotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni zikiwa na lengo la kukusanya fedha kwa ajili kusaidia matibabu na upimaji wa saratani ya shingo ya uzazi kwa wananawake sambamba na kufadhili masomo ya wakunga hapa nchini.