Kalaba apata nafuu, aanza kuzungumza, kula

Muktasari:

  • Akitoa taarifa hiyo leo Ijumaa, Ofisa Uhusiano wa University Teaching Hospital (UTH), Nzeba Chanda, amesema kwamba Kalaba baada ya kupata nafuu amefanikiwa kupata mlo wa kwanza tangu ajali hiyo ilipotokea Jumamosi iliyopita.

ALIYEKUWA nyota wa  TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainfold Kalaba  amerejewa na fahamu na sasa anaweza kuzungumza na kula.

Akitoa taarifa hiyo leo Ijumaa, Ofisa Uhusiano wa University Teaching Hospital (UTH), Nzeba Chanda, amesema kwamba Kalaba baada ya kupata nafuu amefanikiwa kupata mlo wa kwanza tangu ajali hiyo ilipotokea Jumamosi iliyopita.

"Hali ya Kalaba imeimarika sana. Leo alipata mlo wake wa kwanza, yuko na fahamu kabisa na anaweza kuzungumza," amesema ofisa huyo.

"Bado timu ya matibabu inaendelea kumuangalia kwa ukaribu zaidi maendeleo ya afya yake. Tutaendelea kuwajulisha wananchi kwa ujumla kuhusu hali yake.”

Kalaba alipata ajali katika Barabara ya Great North eneo la Kafue huko Zambia, baada ya gari aliyokuwemo kugongana na roli la mafuta.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 37, wakati ajali inatokea  alikuwa abiria katika gari aina ya Mercedes Benz, huku taarifa za awali zikisema alifariki Dunia kabla ya baadaye kuthibitishwa na madaktari kwamba alikuwa hai, lakini ana hali mbaya sana.

Dereva wa gari aliyokuwemo Kalaba alikuwa ni mwanamke aliyetajwa kwa jina la Charlene Mkandawire ambaye alikuwa mke wa rafiki yake ambaye alikutwa amefariki dunia.