Kama utani vile wanaikosa derby Kigoma

KWA sasa mashabiki wa Simba na Yanga wanahesabu saa tu kabla ya kushuka Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kushuhudia timu zao zikivaana katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Simba na Yanga zinakutana kwenye pambano hilo ikiwa ni wiki tatu tangu walipokwaruzana katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika karibuni.

Hilo ni pambano la kwanza kwa watani kukutana mjini Kigoma. Pia ni la kwanza katika michuano ya ASFC kuzikutanisha katika fainali tangu ilipobadilishwa jina kutoka Kombe la FA.

Hata hivyo, bahati mbaya vigogo hao wanakutana kwenye pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Ahmed Aragija na wasaidizi wake Frednand Chacha, Mohammed Mkono na Elly Sasii atakayekuwa wa akiba, kuna baadhi ya wachezaji wa timu hizo watalikosa kama masihara vile.

Baadhi ya wachezaji waliokipiga kwenye mechi zilizopita za Kariakoo Derby  ile ya Novemba 7, mwaka jana; Januari 13, mwaka huu katika Kombe la Mapinduzi na ya Julai 3 watakosekana Kigoma kwa sababu mbalimbali.


METACHA MNATA - YANGA

Huyu ni mmoja wa wachezaji waliokuwa nguzo na kipa tegemeo wa Yanga, lakini utovu wa nidhamu aliouonyesha siku za karibuni kabla ya Ligi Kuu kufika tamati kimemfanya awe kwenye nafasi kubwa ya kulikosa pambano hilo.

Metacha huenda akalikosa pambano hili, kwani Kocha Nasreddin Nabi ameonekana kumuamini zaidi Farouk Shikhalo ambaye huenda akasaidiana na Ramadhani Kabwili aliyechezeshwa mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji na hata kwenye msafara wa Kigoma inaelezwa mchezaji huyo hayupo kabisa.

Kwa namna hali ilivyo ni wazi kipa namba moja kwa pambano la kesho huenda akaanza Shikhalo ambaye alikuwepo kwenye mchezo uliopita wa derby ya ligi na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, huku Ramadhabi Kabwili akianzia benchi ili likitokea la kutokea iwe rahisi kwake kuokoa jahazi.


IBRAHIM AJIBU - SIMBA

Kiungo mshambuliaji huyo wa Yanga hatakuwepo kwenye pambano hilo la Kigoma. Hii ni kwa sababu alishajiondoa mazima Msimbazi hata kabla Ligi Kuu haijafika tamati.

Katika mechi za awali za ASFC kwa Simba, Ajibu alikuwa akipewa nafasi ya kucheza, lakini kwa fainali hii mwamba huyo aliyewahi kukipiga Yanga na kuwa nahodha hatakuwepo Kigoma akiungana na weachezaji wengine ambao wanalikosa pambano hilo.

Hata hivyo, kutokuwepo kwa Ajibu wala sio pengo kwa Simba kwani wachezaji wenye kucheza nafasi kama yake katika kikosi cha Simba wamejaa tele na wamekuwa wakiitenda haki kiasi cha kulisahaulisha jina la fundi huyo wa mpira.


YASIN MUSTAFA - YANGA

Tangu awe majeruhi, beki huyu wa kushoto hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu na pambano hilo pia huenda akalikosa kama alivyolikosa lililopita.

Beki huyo aliyeonyesha uwezo mkubwa kwenye pambano la kwanza la Ligi Kuu Bara la Simba na Yanga lililopigwa Novemba 7, mwaka jana, huenda nafasi yake ikaendelea kuzibwa na Adeyun Saleh.

Kwa Yanga ni pigo kubwa kumkosa Yasin kwenye pambano kama hilo ambalo ni la kuamua hatima ya ubingwa wa michuano ya ASFC hasa baada ya kulikosa lile la Ligi Kuu Bara lililotwaliwa na Simba msimu wa nne mfululizo.


MICHAEL SARPONG - YANGA

Mshambuliaji huyo mwenye mwili jumba na ambaye alifunga bao la kuongoza kwenye Kariakoo Derby ya Novemba, 7 mwaka jana, ana nafasi ndogo ya kulicheza pambano la Kigoma.

Sarpong aliyekuwa ametibuana na kocha wake, Nabi, huenda akalikosa pambano la kesho licha ya kwamba inaeleza msala wake Jangwani, ulishamalizwa kama ilivyokuwa nahodha wake, Lamine Moro ambaye alianza kuitumikia Yanga dhidi ya Dodoma Jiji wakati wa kufunga msimu wa Ligi Kuu.

Kukosekana kwa Mghana huyo sio pigo kubwa kwa Yanga kutokana na ukweli kwenye mechi yao iliyopita ya derby, nafasi yake ilizibwa vilivyo na Yacouba Songne na moto alioupeleka sambamba na wenzake waliipa ushindiYanga dhidi ya Wekundu wa Msimbazi.


JONAS MKUDE - SIMBA

Kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita, hata pambano la Kigoma litampita kiungo huyo wa kikosi cha Simba.

Nahodha huyo wa zamani wa Msimbazi na mchezaji mwandamizi katika kikosi cha Simba hawezi kucheza pambano la kesho kwa vile bado anatumikia adhabu yake ya kusimamiwa na uongozi kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Kesi yake inaelezwa ingeisha mapema kama angekubali kwenda kupimwa hospitali, lakini jamaa anadaiwa alichomoa na sasa anasubiri msimu mpya uanze ajue mustakabali wake kikosini.

Mkude aliyeanza kucheza Kariakoo derby tangu 2012 akiwa ndiye mchezaji mzoefu wa mechi hizo za watani, kesho atakuwa mtazamaji tu, lakini bahati nzuri ni kwamba kuna majembe ya maana Msimbazi yanayoweza kuziba pengo lake.

Kuna Taddeo Lwanga na Mzamiru Yasin na hata Said Ndemla ambao wana uwezo wa kucheza nafasi yake kwa ufanisi na kuipa timu matokeo mazuri mbele ya Yanga, ingawa mashabiki wa Simba wataendelea kummisi, kwani huwa anazijulia sana mechi za namna hii.