Kambi ajiengua ufadhili Ndanda FC

Muktasari:

Mmoja wa wakurugenzi wa Ndanda FC ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha soka mkoani hapa (Mtwarefa), Athuman Kambi ametangaza kujitoa kuifadhili timu hiyo kwa kile alichokieleza kuwa na hali mbaya kifedha kwa upande wake

Mtwara. Mmoja wa wakurugenzi wa Ndanda FC ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha soka mkoani hapa (Mtwarefa), Athuman Kambi ametangaza kujitoa kuifadhili timu hiyo kwa kile alichokieleza kuwa na hali mbaya kifedha kwa upande wake.

Timu hiyo ina jumla ya wakurugenzi 17 lakini Kambi ndiye amekuwa mfadhili mkuu aliyesimama na timu kwa kipindi kirefu sasa huku wengine wakiwa hawashiriki kwa lolote.

“Hali imekua ngumu zaidi tuko kwenye dirisha dogo, mimi binafsi nilijitahidi kadri ya uwezo wangu sasa nimeshindwa, leo tunacheza mechi na Fountain Geti kuanzia leo baada ya mechi mimi binafsi kwa suala la uwezeshaji wa timu ya ndanda uwezo wangu utakuwa umekomea pale na uwezo wangu umeishia pale” amesema Kambi.

Amesema timu bado haiko kwenye hatua mbaya sana na iwapo itashindwa kwenda Mbeya kweye mechi ya Januari 8, 2022 timu itashushwa madaraja mawili na wasipojitokeza watu wa kusaidia basi wana Mtwara watakuwa wameipoteza timu  hiyo.

Kambi amefafanua kuwa timu hiyo kwa sasa ina hali mbaya kifedha hata basi ambalo wanalitegemea kwa usafiri ni bovu linahitaji sio chini ya Sh3.5 millioni kwa ajili ya matengenezo.

Hata hivyo basi hilo hilo limewekwa bondi kwa kiasi cha sh28 millioni kwa ajili ya mikopo ya kuiwezesha timu kusafiri kushiriki mechi mbalimbali na mahitaji mengine huko nyuma.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa walipata nguvu ya kukopa pesa hizo baada ya kusikia kuwa bandari ina mpango wa kuinunua timu hiyo hata hivyo kwa bahati mbaya mpango huo haujafika kokote.

Ndanda ilishuka daraja mwaka 2019 na mwaka huu inashiriki Ligi ya Championship.

 “Juzi hapa hata hela ya kula tulikuwa hatuna tulisaidiwa na bodi ya korosho nchini, (CBT) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara (MAMCU).”amesema Kambi

Kambi amewaomba wanamtwara na wadau wengine wapenda michezo kujitokeza kuinusuru timu hiyo ili isishushwe daraja kwa kushidnwa kushiriki mechi za champion zilizoko mbele yake.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Idrisa Bandari amekiri kupokea taarifa za kukaa pembeni kwa Mkurugenzi huyo na kusema kuwa ameahidi kuwasilisha maandishi rasmi kwa timu.

“Itatuumiza na inaweza kutuvuruga sana yule ni mtu amabye ukiitaja Ndanda unamwangalia yeye kwa kiasi kikubwa tangu ikiwa madaraja ya chini, mkoa, kanda,, ligi kuu hadi championship” amesema Bandari.

Amesema baada ya taarifa hizo walichukua hatua ya kukaa mkurugenzi huyo ili asitishe uamuzi, lakini kwa vile amesema hali yake ngumu kifedha wameshindwa kumlazimisha kwa sababu na wao wameona jinsi gani aliitoa kusaidia timu kwa kipindi chote.

“Kama timu ni pigo kubwa niwaombe watu wa Mtwara kuja kumpata mtu kama yule itachukua muda, ni nafasi watu wa Mtwara, Serikali na wadau waisaidie timu, kama mtu mmoja ameamua kukaa pembeni” amesema Kambi

Akizungumzia mechi ya Mbeya anasema itakua ngumu kwa sababu siku zote Kambi ndie amekuwa msaada mkubwa kila inaptokea safari kama hiyo.

“Safari ile tunahitaji Sh9.8 millioni, kikawaida Kambi hapo angetoa hadi Sh6 millioni na nyingine zingetolewa na wengine kidogo kidogo sasa anakaa pembeni tutafanyaje” amehoji Bandari.

Akizungumzia mchezo wa kesho Januari Mosi 2022 kati yao na Fountain Gate amesema wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo vijaan wako katika hali nzuri