Karata ya kwanza ya Ngorongoro leo Afcon

Tuesday February 16 2021
Karata pic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kikosi cha timu ya Taifa (U-20), Ngorongoro Heroes kinaanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye fainali za Afcon kwenye mchezo wao wa kundi C dhidi ya Ghana utakaopigwa saa 1 usiku Uwanja wa Stade Municipal Nouadhibou, leo.

Washambuliaji wa kikosi cha Ngorongoro Heroes, Kelvin John ‘Mbape’ na Abdul Suleiman wamekuwa katika kiwango bora kwenye mechi za kirafiki walizocheza kabla ya kuondoka nchini.

Kocha wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema anatambua ugumu wa mashindano hayo lakini kupata mechi za kirafiki ana imani zimewasaidia vijana wake.

“Tunaenda kucheza na timu ngumu, lakini nina imani maandalizi ya mechi za kirafiki zimetusaidia kuangalia kiwango cha wachezaji wangu, siangalii sana matokeo ambayo nimeyapata zaidi ni kiwango.

“Kikosi changu kipo vizuri na nina imani kabisa tunafanya vizuri katika mechi zetu zote ambazo tunacheza.”

Nahodha Kelvin John ‘Mbape’ alishukuru kwa maandalizi ambayo waliyapata kwa muda wote waliokuwa kambini na kuahidi kurudi na kombe nyumbani.

Advertisement

Baada ya mchezo huo Ngorongoro Heroes watakuwa na mechi nyingine dhidi ya Gambia (Februari 19) na mchezo mwingine dhidi ya Morocco utakaopigwa Februari 22 katika kundi lao la C.

Advertisement