Karia, Mangungu wafunguka ishu ya Kibu, Uhamiaji yaanika kila kitu

SIKU chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene kutangaza kumpa uraia, straika mpya wa Simba, Kibu Denis ambaye Mwanaspoti liliwahi kukudokeza alikuwa na utata wa uraia wake, klabu yake na Shirikisho la Soka nchini (TFF) limevunja ukimya huku Idara ya Uhamiaji ikifafanua.

Kibu alikuwa kwenye sintofahamu juu ya uraia wa wake hasa baada ya kusajiliwa na Simba msimu huu, baada ya kupenyezewa alikulia kwenye kambi za wakimbizi kabla ya kujichanganya mtaani.

Inaelezwa sakata hilo la uraia pia lilichangia kutotambulishwa kwake rasmi kwenye Siku ya Simba day kama ilivyokuwa kwa wenzake, ingawa uongozi wa Simba ulifafanua kuwa, alisahaulika tu na MC aliyekuwa akiita wachezaji kwa siku hiyo, yaani Joseph Haule ‘Profesa Jay’ ndio maana katika mechi dhidi ya TP Mazembe alianzishwa, huku akishindwa kutumika kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na mbili za Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, baada ya danadana nyingi juu ya sakata la mchezaji huyo, majuzi Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ilitoa taarifa ikieleza Kibu amepewa uraia wa Tanzania.

“Kufuatia Mamlaka aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwa mujibu wa sheria ya uraia, sura ya 357 (Rejeo la 2002), baada ya kupokea ombi lililoletwa kwake na TFF, amempa uraia wa Tanzania mchezaji wa mpira wa miguu, Kibu Denis Prosper, Sept. 30, 2021”, ilieleza taarifa ya wizara.

Kibu aliwahi kukipiga Geita Gold ilipokuwa Daraja la Kwanza (FDL) kabla ya kusajiliwa Mbeya City na kung’ara nayo msimu uliopita kabla ya hivi karibuni kuitwa na kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Julai 13 dhidi ya Malawi Uwanja wa Mkapa.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema walimuombea Kibu uraia kwa kuwa walikuwa wakimhitaji kwenye medani ya soka nchini.

“Sisi tumemuombea Kibu uraia kwa kuwa tunamhitaji, kwa maelezo mengine ni jukumu la Uhamiaji,” alisema Karia kwa ufupi bila kutaka kufafanua kabla ya hapo alikuwa raia wa nchi gani na ilikuwaje alicheza soka kwa miaka yote na hata kuitwa Stars ilihali hakuwa raia wa nchi.

Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk. Anna Makakala alisema kuna taratibu za mtu kuomba uraia na Waziri ana mamlaka ya kisheria kumpa mtu uraia, kama ilivyotokea kwa Kibu, huku Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema changamoto ya usajili wa Kibu ilikuwa ni kuonekana asili yake kukinzana.”

“Mtu anaweza kuhamisha uasili wa wazazi wake baada ya miaka 18, kwa Kibu ilikuwa tofauti kidogo, japo sasa amekamilisha na ataitumikia Simba kama mchezaji mzawa ingawa wenye kulizungumzia zaidi suala lake ni mamlaka za serikali,” alisema Mangungu bila kufafanua alikuwa raia wa nchi gani. Hata hivyo Mwanaspoti ilidokezwa kuwa Kibu ambaye inaelezwa hati yake ya kusafiria inaonyeshwa amezaliwa Mbeya alikuwa akihusishwa na Ukongoman.

Baadhi ya nyota wa zamani wa Simba, Thomas Kipese na Moses Mkandawile kwa nyakati tofauti jana walisema kuna namna kwenye suala la Kibu.

“Kibu amecheza Mbeya City msimu mzima na hata timu ya taifa pia amewahi kucheza na suala la uraia wake halikuonekana hadi aliposajiliwa Simba, inaonekana kulikuwa na umakini mdogo,” alisema Kipese huku akimtolea mfano mmoja wa nyota wa Simba wa zamani ambaye aliwahi kukumbana na sakata kama la Kibu.

Wachezaji waliwahi kuingia kwenye utata wa uraia ni pamoja na Damian Kimti na Said Maulid ‘SMG’ waliokuwa wakituhumiwa awali kuwa ni raia wa Burundi na DR Congo.

Kipese, alisema kinachohitajika ni umakini zaidi, ili mambo yaliyojitokeza kwa Kibu yasiwe na muendelezo.

Wakati Mkandawile ambaye mbali na soka aliwahi kufanya kazi Uhamiaji kati ya mwaka 1978- 1980 akibainisha huenda kulikuwa na tatizo katika suala la kujua sheria ya uraia katika ishu ya Kibu.

“Suala la Kibu linadhihirisha nguvu ya hizi timu mbili za Simba na Yanga, kama angebaki Mbeya City huenda yasingetokea, japo changamoto nyingine kwa watu wa mikoa iliyo mipakani kuna muingiliano sana.

“Mimi binafsi niliwahi kuhusishwa ni raia wa Malawi eti tu jina la Mkandawile pia lipo Malawi, lakini mimi ni Mngoni, hivyo ishu ya Kibu ni suala la kufahamu sheria ya uraia, ila muhimu namshauri Kibu apige kazi tu baada ya sakata lake kumalizika” alisema kipa huyo wa zamani wa kimataifa.