Kaze ashauriwa kukaa na wachezaji

STAA wa zamani wa Yanga, Ally Mayay amemshauri kocha Cedrick Kaze kuanzisha programu ya mchezaji mmojammoja ili kuinua viwango vyao alivyoviona vimeporomoka tofauti na mechi saba za nyuma.

“Kaze afanye kama alichofanya kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa ambaye alianza kumrejesha mchezaji mmojammoja kwenye mstari, kwani tayari alishawajua kwamba wana uwezo, hiyo programu aifanye ili Yanga irejee kwenye mstari hasa mzunguko wa pili ambao ni wa kuvuna kilichopandwa,” alisema Mayay.

Lakini, akasema hajaona kama Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Yacouba Songne wanafiti viwango vya washambuliaji walioondoka kama Amissi Tambwe, Khamis Kiiza na Heritier Makambo ambao walipaswa kulinganishwa

nao kiuwezo.

“Ubora wa mchezaji lazima uufananishe na wale walioondoka, ukiwaangalia hao bado hawajafikia uwezo wa Tambwe, Kiiza na Makambo, tatizo lingine lipo kwa mabeki mfano Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto kila wakati wanarudia makosa yao.”

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alimkingia kifua Kaze kwamba anatakiwa kupata nafasi ya kutengeneza kikosi, hivyo mashabiki wa Yanga wasitarajie kuona kikosi bora kwa msimu huu, ingawa alikiri kila mchezaji aliyepo ni bora.

“Nazungumza kiufundi maana ni mchezaji, najua nini kinaisumbua Yanga, kelele nyingi zitamchanganya Kaze, viongozi watoe tamko la kumlinda kocha kwa sababu alianza na kutengeneza safu ya ulinzi, maana yake ni kwamba kama timu haina kombinesheni isiwe inafungwa ili kuwaondoa wachezaji mchezoni ama kujiamini, ndio maana ilikuwa inafunga bao mojamoja mechi nyingi,” alisema na aliongeza kuwa:

“Kwanza naanza kumpongeza Kaze hadi sasa Yanga kuongoza ligi, mbona Simba imefungwa mechi mbili hakuna kelele na kama watamfukuza itakuwa ngumu kupata timu wanayoitaka, ndio maana anabadili kikosi ili kujua pacha gani zitakuwa bora zaidi, mashabiki waambiwe ukweli kwa maana ya kuwa wavumilivu ili baadaye waje wafurahie matunda.”