Kaze atimuliwa Yanga, benchi la ufundi lavunjwa

BAADA ya kuanza vibaya kwa timu yao katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, uongozi wa klabu ya Yanga usiku huu wa leo Machi 7 umeamua kulivunja benchi lake la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Cedric Kaze.

Yanga imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania ambayo ilikuwa ni mechi ya sita kwenye mzunguko wa pili wakiambulia pointi saba pekee wakidondosha alama 11 baada ya kushinda mechi moja, sare nne na kipigo moja.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo usiku wa leo Machi 7 imeeleza kuwa imeachana na kocha Cedric Kaze aliyesaini mkataba wa kutitumikia miaka miwili Oktoba 16, 2020 , msaidizi wake Nizar Halfan, kocha wa makipa Vladimir Niyonkuru na ofisa usalama wa klabu, Mussa Mahundi.

"Klabu ya Yanga inawashukuru kwa utendaji wao katika kipindi walicho itumikia klabu na tunawatakia kila la kheri," imeeleza taarifa hiyo.

Kaze tangu akabidhiwe timu hiyo ameongoza mechi 18 akishinda 10, sare 7 na amepoteza 1.

Uongozi wa klabu hiyo umewataka wapenzi, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo katika kipindi ambacho wanafanya utaratibu wa kupata benchi jipya.

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili yanga imecheza ugenini dhidi ya Prisons na kutoka sare ya bao 1-1, Mbeya City 1-1, Kagera Sugar 3-3, ikashinda dhidi ya Mtibwa 1- 0 na kufungwa na Coastal Union mabao 2-1.