Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kenya, Tanzania na Uganda zaweka historia CHAN 2024

Muktasari:

  • Kenya imekuwa moja ya timu zilizoshangaza mashindano haya baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza na kuongoza Kundi A. Harambee Stars ilikusanya pointi 10 na kuzizidi kete Morocco na Zambia nyuma yao.

Timu za taifa za Kenya, Tanzania na Uganda zimeandika historia mpya katika soka la Afrika baada ya zote kwa pamoja kufuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 huku wakiongoza makundi.

Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano haya, mataifa matatu wenyeji wa pamoja yamefanikiwa kupenya hatua ya mtoano, jambo linaloibua sura mpya kwenye ramani ya soka Afrika.

Hatua hiyo imezidi kuimarisha kaulimbiu ya mashindano haya ya “Pamoja”, ikionekana si tu katika mgawanyo wa majukumu ya uandaaji, bali pia katika mafanikio ya kila nchi uwanjani.

Mashabiki wamekuwa sehemu ya mafanikio haya kwa kujitokeza kwa wingi na kuunda mazingira yenye hamasa kwenye viwanja vitatu vya Kasarani jijini Nairobi, Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na Mandela jijini Kampala.

Kenya imekuwa moja ya timu zilizoshangaza mashindano haya baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza na kuongoza Kundi A. Harambee Stars ilikusanya pointi 10 na kuzizidi kete Morocco na Zambia nyuma yao.

Ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Zambia katika uwanja wa Kasarani kupitia mfungaji Ryan Ogam dakika ya 75 uliwapa heshima kubwa na kuamsha ari ya mashabiki waliokuwa wamefurika kushuhudia mechi hiyo.

Kocha Benni McCarthy amesifiwa kwa kuibadilisha timu hiyo na kuwapa wachezaji imani ya kupambana na wakongwe wa soka la Afrika. Nidhamu ya kiuchezaji na uwezo wao wa kutumia nafasi chache walizopata umeibua hofu kwa wapinzani na matumaini kwa mashabiki wa nyumbani ambao sasa wanaamini timu yao inaweza kusonga mbele zaidi.

Tanzania nayo imekuwa kivutio kikubwa baada ya kuibuka kinara wa Kundi B kwa pointi 10. Taifa Stars ilishinda mechi tatu kati ya minne, na sare pekee waliyoipata ilikuwa dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mechi ya mwisho ambayo haikuwa na umuhimu.

Kutinga hatua hiyo kwa Taifa Stars kumetokana na uzoefu wa wachezaji wake katika mashindano ya kimataifa, uimara wa safu ya ulinzi na nidhamu ya kiufundi iliyoweka timu hiyo katika kiwango bora.

Kwa Uganda, hatua hii ni historia mpya baada ya kushindwa mara sita mfululizo kuvuka hatua ya makundi katika mashindano ya CHAN.

Safari hii The Cranes walionyesha ukomavu wa kiuchezaji na kupambana hadi dakika za mwisho kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Afrika Kusini kwenye mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Mandela.

Katika mechi hiyo ambayo ilichezwa juzi, Jumatatu, Uganda ilianza vizuri kwa kufunga mapema kupitia Jude Ssemugabi, lakini baadaye Afrika Kusini ilirejea na kufunga mabao matatu.

Mashabiki wa Uganda walidhani ndoto yao imeota mbawa, lakini dakika za majeruhi Rogers Torach alisawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya Allan Okello kufunga la pili. Sare hiyo iliwaweka kileleni mwa kundi na kuipa timu hiyo nafasi ya kwanza kufika robo fainali.

Matokeo hayo yamezua matumaini mapya kwa mashabiki wa Uganda waliokuwa wamelazimika kuvumilia miaka mingi ya kushuhudia timu yao ikitolewa mapema. Sasa wanaamini kuwa kikosi hicho kinaweza kuandika sura mpya ya mafanikio katika mashindano haya. Jumamosi usiku watakuwa nyumbani tena kuchuana na mshindi wa pili wa Kundi D.

Ratiba ya robo fainali inaonyesha Kenya ikimenyana na Madagascar jijini Nairobi, Tanzania dhidi ya Morocco jijini Dar es Salaam, mshindi wa Kundi D atakutana na Algeria katika Uwanja wa Amaan Zanzibar, huku Uganda wakicheza na mshindi wa pili wa Kundi D jijini Kampala.