Sasa ni Taifa Stars dhidi ya Morocoo kwa Mkapa
Muktasari:
- Wakati Kenya ikiendeleza ubabe kwenye kundi hilo na kufikisha pointi 10 sawa na Taifa Stars iliyopo kundi B, upande wa pili kwenye Uwanja wa Nyayo jijini hapo hapo Nairobi.
Dar es Salaam. Hatimaye imefahamika kuwa Taifa Stars itacheza dhidi ya Morocco Agosti 22 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024 baada ya mechi za kundi A kumalizika leo Jumapili huku Kenya ikiweka rekodi.
Timu ya taifa la Kenya, iliweka rekodi ya kumaliza kinara katika kundi A baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zambia, lililofungwa dakika ya 75 na Ryan Ogam kwenye uwanja wa kimataifa wa Moi, Nairobi.
Wakati Kenya ikiendeleza ubabe kwenye kundi hilo na kufikisha pointi 10 sawa na Taifa Stars iliyopo kundi B, upande wa pili kwenye Uwanja wa Nyayo jijini hapo hapo Nairobi, Morocco iliidhibu DR Congo kwa mabao 3-1, hivyo kumaliza hatua hiyo ikiwa nafasi ile ile ya pili katika mchezo uliokuwa mkali na wa kuvutia.
Kwa matokeo hayo, Kenya itacheza dhidi ya Madagascar ambayo yenyewe ilivuna pointi saba na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi B, ambalo limeongozwa na Taifa Stars kwenye mchezo utakapoigwa Uwanja wa Moi nchini Kenya.
Morocco ambayo imemaliza nafasi ya pili kundi A, sasa itasafiri kuja Tanzania kukabiliana na Taifa Stars ambayo ilitinga hatua hiyo kabla ya mechi za mwisho za hatua ya makundi baada ya kushinda mechi tatu mfululizo.
Morocco na Stars ni mchezo ambao unatarajiwa kuwa mkali kutokana na ubora wa timu zote, lakini nafasi za kiwango cha ligi zao ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye ubora.
Katika hatua ya makundi, Morocco imeshinda mechi tatu huku ikichapwa moja dhidi ya Kenya iliyokuwa pungufu kwa bao 1-0, imefunga jumla ya mabao manane sawa na wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mechi, imeruhusu mabao matatu.
Taifa yenyewe imeshinda mechi tatu na kutoa sare moja, imefunga jumla ya mabao matano sawa na wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mechi huku ikiruhusu bao moja tu ndio timu yenye safu ngumu zaidi ya ulinzi kwa kuangalia timu zote katika hatua hiyo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Taifa Stars kukutana dhidi ya Morocco katika michuano ya CHAN 2024, Morocco imetwaa mara mbili ubingwa wa CHAN 2024 huku Stars ikitinga hatua hii kwa mara ya kwanza baada ya kushiriki mara tatu.
Kijumla katika mashindano yote, Morocco na Tanzania zimekutana mara saba, Morocco imeshinda mara sita huku Stars ikishinda mara moja.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Machi 26 mwaka huu katika kinyanganyiro cha kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia na Stars ilipoteza kwa mabao 2-0, hata hivyo juzi kocha wa Stars Hemed Morocco alisema hana hofu na timu yoyote ambayo atakutana nayo hatua ya robo fainali kwa kuwa kikosi chake kipo imara.