Kiatu cha 3.7 milioni kumbeba Geay Boston Marathon

Muktasari:

  • Mbio hizo zitakuwa majira ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki huku Geay akiwa na kumbukumbu nzuri ya kushika nafasi ya pili mwaka 2023, akitumia muda wa masaa 2:06:04 nyuma ya Mkenya Evans Chebet aliyeongoza kwa 2:05:54.

Arusha. Mashindano ya mbio za Boston Marathon yanatazamiwa kutimua vumbi leo Aprili 15 nchini Marekani huku mwanariadha wa Kimataifa kutoka Tanzania, Gabriel Geay akiwa ni miongoni mwa nyota ambao wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

Mbio hizo zitakuwa majira ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki huku Geay akiwa na kumbukumbu nzuri ya kushika nafasi ya pili mwaka 2023, akitumia muda wa masaa 2:06:04 nyuma ya Mkenya Evans Chebet aliyeongoza kwa 2:05:54.

Katika kuhakikisha anaendeleza pale alipoishia mwaka jana, nyota huyo ambaye anashikilia rekodi ya taifa ya mbio ndefu kwa muda wa 2:03:00 amepanga kuvaa kiatu chenye thamani ya shilingi  3.7  milioni akiamini ubora wa kiatu hicho utamfanya kuendelea kuwatimulia vumbi nyota wenye rekodi za dunia akiwemo Eliud Kipchoge wa Kenya.

Adidas dizero Adios Pro Evo 1,rangi nyeupe yenye michirizi ambayo inauzwa dola za Kimarekani 1,474 sawa na Sh3.7 milioni za Kitanzania ndicho Geay atavaa  leo huku akibeba mioyo ya Watanzania zaidi ya milioni 60, ambao wako nyuma yake wakimwombea ushindi.

Akizungumza na Mwananchi moja kwa moja kutoka Marekani nyota huyo amesema maandalizi yake yamekamilika, hakuna tatizo la hali ya hewa hivyo kilichobaki ni kufanya kile ambacho amekuwa akikifanya mara zote kwa maana ya kushinda na kuipeperusha vyema bendera ya nchi.

"Kila kitu kiko sawa kuanzia kwenye maandalizi na mazingira kwa ujumla hata ukiangalia kiatu ambacho nitakitumia cha mdhamini wangu kina ubora mkubwa naamini nitafanya vizuri.

"Ili kushinda mbio kubwa unahitaji kuwa na vitu ambavyo vinakuongezea morali mwenyewe mwanariadha ikiwemo viatu vyenye ubora wa kukimbilia",

“Natarajia nitakimbia vyema japo siwezi kusema nitashinda moja kwa moja kwani sijui wapinzani wangu wamejiandaa vipi lakini nimefanya maandalizi ya kutosha kufanya hivyo”, amesema Geay.

Mwanariadha huyo ambaye alimaliza wa saba katika mashindano ya Dunia mwaka 2022, ameongeza kuwa kama mambo yataenda vizuri jinsi ambavyo amepanga anaamini leo ataipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa kwa kuongoza na kuwashinda wababe wa mbio hizo kwa dunia.

“Natambua kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wengine hivyo nimefanya maandalizi ya kutosha kuja kumalizia pale ambapo niliishia mwaka jana ",ameongeza.

Geay ambaye alianza na mbio ndefu za viwanjani (mita 5000 na 10000) baada ya kumaliza Boston Marathon atahamishia katika mashindano ya yatakayofanyika Paris Ufaransa, Julai mwaka huu.