Kilichoiponza Simba hiki hapa

Dar es Salaam. Kukosekana kwa ubunifu na ufanisi kwa Simba hasa safu yake ya kiungo katika kujenga mashambulizi ni sababu kubwa iliyochangia kushindwa kupata ushindi katika mchezo muhimu wa nyumbani wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, juzi.

Pamoja na kuanzisha kundi kubwa la wachezaji wenye asili ya kushambulia, Simba iliondoka patupu kwa kushindwa kufunga bao kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao, jambo linaloiweka kwenye nafasi ngumu ya kupata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano ugenini utakaochezwa Aprili 13 mjini Lubumbashi.

Licha ya kumiliki mpira kwa asilimia kubwa, Simba ilipata wakati mgumu kupenya ukuta mgumu uliocheza kwa nidhamu wa TP Mazembe na hata nafasi chache ilizopata ilishindwa kuzitumia kufunga mabao.

Wachezaji wa Simba hasa waliokuwa wakicheza safu ya kiungo, walipiga pasi nyingi za kwenda pembeni mwa uwanja pindi walipokuwa na mpira jambo lililosababisha TP Mazembe kujipanga kwa haraka na kutibua mashambulizi yao.

Simba licha ya kucheza vizuri kuanzia nyuma hadi katikati, mipango yao ilitibuliwa katika eneo la mwisho la adui, ambapo idadi kubwa ya pasi walizopenyeza langoni mwa TP Mazembe zilinaswa na mabeki.

Takwimu za mchezo wa juzi zilizotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zinaonyesha Simba ilipoteza mpira mara nyingi kuliko TP Mazembe ambapo wachezaji wake walipoteza mpira mara 143 wakati wapinzani wao walipoteza mara 128.

Pia nafasi chache ambazo walipata ndani ya boksi la TP Mazembe walikosa ubunifu na mbinu ya kuzitumia kufunga mabao na kujikuta wakipiga idadi kubwa ya mashuti ambayo hayakulenga lango.

Pamoja na kumiliki mpira, Simba walipiga shuti moja lililolenga lango huku tisa yakishindwa kulenga kwa kutoka nje au kupaa.

Baadhi ya makocha nchini akiwemo kocha nguli aliyewahi kuinoa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Dk Mshindo Msolla, alisema wachezaji wa viungo wa Simba wanapaswa kubadilika katika mechi ya marudiano.

“Kuna nyakati washambuliaji wao hutokea pembeni, hivyo viungo wanatakiwa kwenda kuziba nafasi lakini pia wamekuwa wakipokea mipira umbali wa mita takribani 30 kutoka langoni mwa mpinzani lakini hawajajenga utaratibu wa kupiga mashuti, wakifanya hivyo watafunga mabao mengi. “Kwenye mechi ya marudiano nadhani kikubwa wanapaswa kuichunga zaidi Mazembe pembeni kwani ndiko inakoonekana ina nguvu zaidi,” alisema Dk Msolla.

Kocha wa Prisons Mohamed ‘Adolf’ Rishard alisema ushindi wa Simba ugenini utategemea na namna watakavyoamka siku ya mechi.

“Huenda Simba wanaweza kufanya chochote kule, lakini Mazembe si timu ya kiwango cha juu, wanazijua fujo zote za soka la Afrika, ushindi wa Simba utategemea tu namna siku hiyo wachezaji walivyoamka na kocha amekiandaa vipi kikosi,” alisema Rishard.

Kocha wa Lipuli na nahodha wa zamani wa Simba, Selemani Matola alisema katika mchezo wa juzi Simba ilikosa bahati.

“Kikubwa wamepata suluhu, bado ni faida kwa Simba kwasababu ili Mazembe apite lazima apate goli, Simba wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuhakikisha hafungwi kule Congo,” alisema Matola.

Wakati aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema matokeo ya juzi ni ‘credit’ kwa Simba.

“Tumetoka suluhu na timu iliyowahi kuwa mabingwa wa Afrika, hiyo ni ‘credit’ kwa Simba ingawa watu wengine hawajui, isitoshe bado tuna nafasi nzuri ya kusonga mbele na kucheza nusu fainali,” alisema Rage.

Rage alisema Simba hawapaswi kuruhusu bao ugenini na wapambane kupata bao la mapema ili kujiweka katika mazingira mazuri.