Kilichombeba McTominay Serie A hiki hapa
Muktasari:
- Sababu ya pili ni idadi kubwa ya mabao ambayo amefunga na kupiga pasi za mwisho ambayo yamemfanya awe kiungo aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi hiyo ya Italia.
Napoli,Italia. Juzi Alhamisi ilikuwa siku ya kihistoria kwa Napoli baada ya kutwaa rasmi taji la Ligi Kuu Italia 'Serie A'msimu huu lakini kwa kiungo wake Scott McTominay, kumbukumbu za siku hiyo zitadumu kwa miaka mingi.
Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United aliibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Serie A msimu huu, tuzo ambayo imechukuliwa kwa mara ya kwanza na mchezaji raia wa Scotland.
Sababu mbili zinaonekana kumbeba McTominay hadi akafanikiwa kutwaa tuzo hiyo licha ya miezi kadhaa nyuma kuonekana sio mchezaji anayeweza kuipa mchango mkubwa Manchester United hadi ikaamua kumuuza Napoli kwa dau la Euro 30 milioni (Sh92 bilioni).
Kwanza ni kiwango chake cha uhakika kilicholishawishi benchi la ufundi la Napoli chini ya Antonio Conte kumpa namba ya kudumu kikosini na kuthibitisha hilo, kati ya mechi 38 za Serie A, kiungo huyo amecheza idadi ya michezo 34 huku akikosekana katika mechi nne tu.
Sababu ya pili ni idadi kubwa ya mabao ambayo amefunga na kupiga pasi za mwisho ambayo yamemfanya awe kiungo aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi hiyo ya Italia.
Katika mechi 34 za Serie A, McTominay amefunga mabao 12 na kupiga pasi za mwisho sita.
Ikumbukwe katika mechi 178 za Ligi Kuu England ambazo McTominay aliichezea Manchester United, kiungo huyo alifunga mabao 19 tu.
McTominay hajafunga tu bali pia idadi kubwa ya mabao ambayo amepachika yalikuwa ya kutangulia kwa Napoli ambapo katika mabao 12 aliyofunga, nane yalipatikana wakati timu yake ikiwa na sare ya 0-0 dhidi ya timu pinzani.
Mafanikio hayo yanatokana na kucheza zaidi nafasi ya kiungo mshambuliaji katika timu hiyo chini ya Conte. Katika muda mwingi alioichezea Manchester United, McTominay alicheza katika nafasi ya kiungo mkabaji na kwa timu ya taifa ya Scotland alikuwa anachezeshwa katika nafasi ya mlinzi wa kati.
"Conte alibadilisha mfumo wake ili kumweka katika mazingira bora ya kucheza.
"Katika mfumo wa Conte yeye si mjenzi, ni mshambulizi. Chaguo bora huku ukiwa na nambari tisa kama Romelu Lukaku, ambaye leo anacheza na anatengeneza sana nafasi kwa timu," alisema mwandishi wa habari wa Naples Vincenzo Credendino.
McTominay mwenyewe amesema kuwa siri ya mafanikio yake ni hamu ya kuwapa furaha mashabiki wa Napoli.
“Niliona mashabiki wenye shauku, nilimuona kocha, nikaona wachezaji na nikaona fursa.
"Ninapenda mahali hapa, ninawapenda mashabiki, nawapenda wachezaji wenzangu," alisema McTominay.