Kipigo chamtaafisha Mahrez Algeria
Muktasari:
- Mahrez amewashukuru mashabiki wote na kuweka wazi kuwa huu ulikuwa wakati sahihi wa kupisha kizazi kipya cha wachezaji kuiongoza timu hiyo.
Nahodha na mshambuliaji wa Algeria, Riyad Mahrez, ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya safari ya kihistoria na timu hiyo.
Mahrez ametangaza uamuzi huo baada ya Algeria kuondolewa kwenye Kombe la Dunia la FIFA 2026 katika hatua ya 32 bora kufuatia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Uswisi.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 35 anayechezea klabu ya Al-Ahli ya Saudi Arabia, anaondoka kikosini akiwa nguzo na alama kubwa ya soka nchini Algeria.
Katika kipindi cha miongo miwili ya utumishi wake, Mahrez ameichezea timu ya taifa michezo 119, akifunga mabao 40 na kutoa pasi za mabao (assists) 45, takwimu zinazomfanya kuwa mfungaji bora wa pili wa muda wote wa nchi hiyo.
Moja ya mafanikio makubwa yanayomfanya kukumbukwa milele ni kuiongoza Algeria akiwa nahodha kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2019, pamoja na kuwika kwenye michuano mikubwa ya Kombe la Dunia.
Mahrez amewashukuru mashabiki wote na kuweka wazi kuwa huu ulikuwa wakati sahihi wa kupisha kizazi kipya cha wachezaji kuiongoza timu hiyo.