Kisa Afcon 2027, TFF yapewa angalizo la afya

Muktasari:

  • Dk Kwesi ameyasema hayo  jana Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo  ya huduma za afya kabla nje ya Hospitali  na kukabiliana na maafa na dharura.

Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Huduma za Dharura Wizara ya Afya Dk Elias Kwesi amelielekeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kutowatumia watu wasio na ujuzi wa masuala ya dharura na maafa kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Dk Kwesi ameyasema hayo  jana Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo  ya huduma za afya kabla nje ya Hospitali  na kukabiliana na maafa na dharura.

Mafunzo hayo yanafanyika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) yakifadhiliwa na Shirika kutoka nchini Uturuki (TiKA) ikihuisha wataalamu zaidi ya 700  kutoka maeneo mbalimbali nchini.

"Nchi yetu itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027, niwaombe TFF  vigezo vya watoa huduma wa afya  kwenye mashindano vizingatiwe, tutajenga heshima yetu  ngazi ya michezo"alisema.

Dk Kwesi alielekeza kuwa  watu waliopata mafunzo ndio watoe huduma za dharura  kwa wachezaji  na siyo deiwaka.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas, Profesa Emmanuel  Balandya  alisema mafunzo yaliyoanza kutolewa na chuo hicho ya masuala ya huduma za dharura na majanga  ni maandalizi ya utayari wa kukabiliana na majanga.

Miongoni mwa viasharia vya uwezekano wa kutokea majanga ni mkusanyiko mkubwa wa watu, mwaka 2027  tunatarajia kuandaa  mashindano ya  makubwa  ya AFCON  na  maelefu ya watu watashiriki,"alisema.