Klopp amfagilia Sturridge

Muktasari:

  • Ni baada ya kuonyesha kiwango jana

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amemfagilia mshambuliaji wake Daniel Sturridge, akisema tangu amemfahamu hajawahi kumuona akicheza kwa kiwango cha juu kama alivyofanya juzi dhidi ya PSG ya Ufaransa.

Liverpool iliikaribisha PSG na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, Sturridge ndiye aliifungia timu yake bao la kuongoza dakika ya 30 kabla ya James Milner kuongeza la pili kwa penalti dakika ya 36 kutokana na mshambuliaji huyo kuchezewa faulo na mtokea benchi Roberto Firmino akipa ushindi dakika ya 90.

Klopp alisema PSG iliwawekea ulinzi maalumu washambuliaji wao Sadio Mane na Mohammed Salah na kuwapuuza wengine akiwemo Sturridge aliyewadhibu kabla Firmino, aliyeingia badala yake dakika ya 72 akaihakikishia Liverpool ushindi.

“Sturridge amecheza mchezo huu katika kiwango cha juu sana ambacho sijapata kumuona nacho, alikuwa akijiamini na alifanya maamuzi sahihi muda wote,” alisema Klopp.

Kocha huyo aliongeza kusema kuwa atampa nafasi ya kutosha mshambuliaji huyo iwapo atakuwa fiti kwani muda mrefu alikuwa akiutumia kuwa nje kutokana na kukabiliwa na majeruhi ya mara kwa mara ya goti na msuli.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kila timu za kundi C, mbali ya Liver na PSG timu nyingine za kundi hilo ni Napoli ya Italia na Red Star Belgrade ya Serbia.