Kocha DR Congo atabiri ubingwa Afrika
Muktasari:
- Desabre amesema pia anadhani bara la Afrika linatakiwa kuongezewa idadi ya timu zinazoshiriki Kombe la Dunia.
Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo, Sébastien Desabre, anaamini kwamba siku zinakaribia kwa timu kutoka Afrika kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia na kumaliza unyonge wa miaka 96 katika mashindano hayo.
Tangu Kombe la Dunia lilipoanzishwa mwaka 1930, hakuna timu ya Afrika iliyowahi kuingia angalau katika hatua ya fainali huku mafanikio makubwa yakiwa ni ya Morocco kufika nusu fainali katika fainali za mwaka 2022.
Lakini kiwango bora kinachoonyeshwa na timu za Afrika katika Fainali za mwaka huu zinazoendelea katika nchi za Canada, Mexico na Marekani, kinamkosha Desabre ambaye anaamini kwamba neema inakaribia kwa Afrika.
Mbali na kutabiri hilo, Desabre amesema pia anadhani bara la Afrika linatakiwa kuongezewa idadi ya timu zinazoshiriki Kombe la Dunia.
"Afrika inaendelea kukua na maendeleo hayo hayatasimama.
"Natumaini mwaka huu, au katika miaka ijayo, timu kutoka Afrika itafanikiwa kutwaa Kombe la Dunia. Kwangu mimi, ni suala la muda tu," alisema Desabre.
Kocha huyo amekiongoza kikosi cha DRC kutinga katika hatua ya 32 bora ya michuano hiyo mikubwa duniani baada ya kukusanya idadi ya pointi nne katika kundi K lililokuwa na timu za Ureno, Colombia na Uzbekistan.
DR Congo ilianza kwa kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Ureno, kisha ikapoteza 1-0 dhidi ya Colombia kabla ya kuichapa Uzbekistan mabao 3-1 katika mechi ya mwisho.
Katika hatua ya 32 bora DR Congo itavaana na England, Julai Mosi mwaka huu.