Kocha Peter Manyika afariki dunia, familia yathibitisha
Muktasari:
- Peter Manyika aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1999 nchini Uganda.
Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika amefariki leo alfajiri na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.
Taarifa kutoka kwa mtoto wa marehemu, Manyika Peter methibitisha kwamba msiba upo nyumbani kwao Mbezi.
"Baba kafariki leo alfajiri, msiba upo nyumbani Mbezi. Kwa sasa ni ngumu kusema vitu vingi bado sijatulia,"amesema Manyika.
Mtunza Hazina wa taasisi ya wachezaji wa zamani Galacticos, Idd Moshi, amesema jambo la msingi kwa sasa ni Watanzania kujua kuhusu msiba huo, mengine wasubiri hadi watakapokaa kikao na familia yake.
"Mwenzetu kafariki leo alfajiri, atazikwa lini bado hatuna taarifa hiyo hadi tutakapokaa na familia yake. Mara ya mwisho kikazi alikuwa na Namungo FC," amesema Moshi.
Mbali na kuitumikia Yanga kama kipa na kocha wa makipa, timu zingine alizowahi kuzitumikia ni Yanga, Ihefu Fc, Singida Fountain Gate, Dodoma Jiji na Namungo.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.