Kule Namungo, huku Ihefu

LIGI Kuu Tanzania bara itaendelea leo Mei 12, 2021 kwa mechi mbili kupigwa katika viwanja tofauti ambapo Namungo itaikaribisha Mtibwa Sugar huku Ihefu wakiwakabili Polisi Tanzania.

Mchezo wa mapema utaanza saa 8:00 mchana katika uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi ambapo Namungo watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.

Mchezo huo utakuwa wa 25 kwa Namungo iliyo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi na alama 32, na mechi ya 28 kwa Mtibwa inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani kwenye msimamo (17) ikiwa na jumla ya alama 28.

Mechi nyingine itapigwa saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Highland Estate Mbalali Mbeya kati ya wenyeji Ihefu na Polisi Tanzania.

Pia mechi hii inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na wenyeji Ihefu walio nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi na pointi 30 wanapambana kukwepa kushuka daraja huku Polisi Tanzania walio nafasi ya nane na alama 37 wakitaka kupanda katika nafasi nne za juu.

Michezo ya mwisho timu hizo kukutana Namungo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Oktoba 19, mwaka jana huku Ihefu na Polisi Tanzania zikitoka suluhu (0-0), Novemba 21 mwaka jana.