Kutoka masumbwi, nyota wa Madola hadi uchungaji
Dar es Salaam. Alikuwa miongoni mwa 'medalist' wa Tanzania kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1982, Zakayo Malekwa na bingwa wa zamani wa Taifa wa uzani wa walter, Somwe Patauli.
Wanamichezo hao sasa ni wachungaji, Malekwa aliyewahi kuvunja rekodi ya Afrika Mashariki ya kurusha mkuki ni mkuu wa pili wa Jimbo la Dongobesh.
Mchungaji huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) anaeleza namna alivyowiwa kufanya kazi hiyo ya Mungu akiwa kwenye timu ya taifa ya riadha.
"Kilikuwa ni kipaji changu kingine, nikiwa kwenye timu ya taifa nilikuwa nafanya injili pia, vilevile nilikuwa mpiga kinanda hodari. Mwaka 1979 nikiwa kwenye kambi ya timu ya Taifa kujiandaa na Olimpiki ya 1980, niliota ndoto ambayo ilinipa maono ya kuandika mashairi ya wimbo wa Lulu uliokuja kuimbwa na kwaya ya Mtoni ya jijini Dar es Salaam," anasimulia.
Akiimba baadhi ya mashairi ya wimbo huo yanayosema Yesu nipeleke kule kwa Baba nikaishi naye kule Mbinguni, kwenye mji wa lulu, milango ya dhahabu, ambao ni miongoni mwa nyimbo zilizovuma miaka ya nyuma. Niliutunga nikawaachia, mimi nikaenda Marekani," anasema Malekwa aliyeingia kwenye riadha mwaka 1974 akiwa jeshini Mgulani JKT.
Mwaka 1976 kwenye mashindano ya Taifa, Malekwa alirusha mkuki umbali wa mita 65 na kuvunja rekodi ya Taifa iliyokuwa ikishikiliwa na James Wanda wa JWTZ na mwaka uliofuatia alivunja ile ya Afrika Mashariki akirusha mita 79.
Mwaka 1982 akiwa na timu ya Taifa iliyoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola na kushinda medali ya shaba akirusha mita 80, akiwa chini ya ulezi wa kocha Mbiza (sasa ni marehemu) na Ernest Salia.
Malekwa alipata nafasi ya kusoma Marekani na kucheza, ambako huko aliweka rekodi ya mita 87 kwenye mashindano ya vyuo vikuu.
"Wakati ule niliingia kwenye rekodi ya nyota bora watano wa dunia na mwaka 1988 ndipo nilistaafu baada ya Michezo ya Olimpiki.
"Nilistaafu riadha kutokana na ratiba, sikuweza tena kusoma na michezo, baada ya masomo yangu, nilirudi jeshini kabla sijaamua kuingia kwenye uchungaji.
"Ni mwaka wa 17 nahudumu huduma hii nikiwa mkuu wa pili wa Jimbo Usharika wa Dongobesh.
"Ni kazi ambayo nimeifanya tangu nikiwa kijana, nilikuwa nikihubiri, napiga vyombo kanisani na pia kutoa huduma ya mashahidi ninayoifanya hadi sasa.
"Japo mwanzoni ilinipa shida kueleweka kwa wanamichezo wenzangu kambini, lakini kadri siku zilivyosonga wengi walielewa nina kitu kwenye injili," anasema Malekwa aliyekuwa muasisi wa kwaya ya Mtoni.
Anasema akiwa Russia kambini ndipo alitunga wimbo wa Lulu na alikuwa na upako tangu zamani alipokuwa kijana alikuwa akihubiri na kushuhudia japo wakati huo alikuwa ni mchezaji wa timu ya Taifa.
Baada ya uchungaji anarudi huku
Malekwa anasema anakaribia kustaafu uchingaji, huku mikakati yake ikiwa ni kuanzisha klabu ya field events akitaka kufufua michezo ya miruko na mitupo.
"Nitaianzishia Dongobesh, wilayani Mbulu, nataka kufufua michezo yote ya mitupo, japo hammer sijawahi kucheza, lakini nao nafikiria niuanzishe kwenye klabu hiyo," anasema.
Michezo mingine ni kurusha tufe, mkuki na kisahani, ingawa pia amesisitiza klabu hiyo itakuwa na michezo yote ya miruko.
"Tunapozungumzia michezo, sio kucheza cheza, huo ni wajibu, hivyo nahitaji kufanya wajibu wangu kwenye michezo ya miruko na mitupo ambayo hapa nchini imesahaulika," anasema.
Somwe Patauli
Bondia huyu nguli wa zamani wa uzito wa welter ambaye enzi zake alifahamika kwa jina la utani la 'Okapi' alijaza mashabiki kwenye mapambano yake wakati huo kwenye kumbi za Relwe Gerezani, DDC Keko, DDC Magomeni Kondoa na Lang'ata Social Hall.
Enzi zake aliwatoa jasho na damu mabondia kama Chuku Dusso (Dancer), Stanley Mabesi na wengine wengi maarufu lakini sasa ni mchungaji, mikono ile iliyotumika kuwatoa damu wapinzani wake ulingoni, sasa inatumika kuwagusa wahitaji.
Ukifika katika Kanisa la Huduma Huru na Ukombozi (JCMC) lililopo Kigamboni Tungi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Patauli ndiye mchungaji akishirikiana na wahudumu wengine wa kanisa akiwamo mama mchungaji, Elikana.
Mkewe anasema alikutana na Patauli akiwa tayari ameacha maisha ya ubondia na kumrudia Mungu baada ya kusomea uchungaji.
"Nilikuwa nasikia tu stori kwamba enzi anapigana alipewa jina la utani Okapi, ambalo hilo jina kwa lugha ya kiswahili ni kisu, alilopewa kutokana na ukali wa ngumi zake ambazo zilifananishwa na kisu," anasimulia Elikana.
Kabla ya kufanya mahojiano, Patauli alifanya maombi na kisha kueleza namna alivyoingia kwenye uchungaji.
"Niliposema nimeokoka kuna watu walifikiri nimechanganyikiwa. Kila mmoja alizungumza lake, wengine walisema tangu lini bondia akaokoka, wapo waliofikiri nimepatwa na janga lililonifanya nitangaze kuokoka.
"Nilipiga magoti nikamwambia Mungu 'kama umeruhusu nifanye kazi yako, basi jina lako lihimidiwe', sikutaka kurudi nilikotoka," anasema.
Anasema alipata neema ya kuokoka na kuacha ngumi 1992, lakini baada ya muda akarejea kwenye ngumi wakati huo akiwa ameokoka.
"Kwa miaka miwili ambayo nilirudi katika ngumi sikufanikiwa kila nilichofanya kilifeli kilikuwa kipindi kigumu kwangu niliona kama majaribu ndipo nikakata shauri nirudi kumtumika Mungu kwa moyo wangu wote," anasema.
Anasema alikata shauri kwenda kusomea uchungaji akaacha kila kitu na kutundika glovu, hakuna aliyeamini, marafiki zake walihisi amechanganyikiwa, lakini yeye aliamua kufanya kazi ya Mungu.
Enzi anacheza, Patauli alikuwa mpinzani wa jadi na Stanley Mabesi 'Ninja', ambaye kwa sasa yuko Uholanzi na inaelezwa huko pia Mabesi ni mchungaji.
"Pambano na Mabesi lilikuwa na ushindani kama ambavyo unaona kwa Simba na Yanga tulikuwa tukicheza ukumbi unajaa, tambo za pambano zinafanyika mwezi mmoja kabla," anasimulia.
Mbali na upinzani wa jadi na Mabesi, Patauli anaeleza namna alivyogomea pambano akiwa kwenye harakati za kuokoka.
"Ilikuwa mwaka mmoja kabla ya kuokoka, tulikwenda Uingereza kucheza pambano nikiwa na Lucas Msomba (marehemu) aliyekuwa akichezea uzani wa juu na Anthony Nyembele ambaye alikuwa akicheza uzani wa chini.
"Tulichukuliwa kwenda kucheza mapambano ya utangulizi kusindikiza la ubingwa Jumuiya ya Madola, ambalo Mkenya, Modest Napuli alikuwa akigombea ubingwa na bondia wa nchi ile.
"Watanzani tulicheza vizuri wote, pale nilipata ofa ya kwenda kucheza na kuishi Ufaransa, kipindi ambacho nilikuwa kwenye harakati za kuokoka, nikagoma kwenda," anasema.
Anasema awali alipoingia katika kazi ya Mungu, changamoto ilikuwa kubwa lakini alijifananisha na Mtume Paulo.
"Paulo alipoamini wengi hawakumkubali kwa walifahamu huyu ametokea sehemu fulani, ndivyo ilikuwa kwangu.
"Wengine waliona kama nadhihaki, wengine hawakuamini, nilipiga magoti nikamwambia Mungu kama umeamua niifanye kazi yako, basi nitendee sawa na fadhili zako, nilifanya maombi ya toba kwani bila toba shetani anakurudisha nyuma," anasema.
Patauli anasema alipookoka alilelewa kiroho kwenye kanisa la Deeper-life kwa kushirikiana na lile la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF).