Ligi Kuu yaanza na machungu ya wadhamini

Muktasari:

  • Gharama ambazo timu nane zitatumia kwenye mechi zao za ufunguzi wa ligi ambazo zitacheza kwenye viwanja vya ugenini nje ya mikoa yao ni kiashirio cha namna timu zitakapokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha za udhamini wa ligi hiyo.

Dar es Salaam. Klabu nane za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeanza kutoa taswira ya nyakati ngumu ambazo ligi hiyo itapita msimu huu kutokana na kukosekana kwa mdhamini mkuu.

Gharama ambazo timu nane zitatumia kwenye mechi zao za ufunguzi wa ligi ambazo zitacheza kwenye viwanja vya ugenini nje ya mikoa yao ni kiashirio cha namna timu zitakapokabiliana na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha za udhamini wa ligi hiyo.

Kupungua huko kwa fedha za mgawo ambao klabu zilikuwa zinapata kutoka kwa wadhamini kunatokana na Ligi hiyo kutokuwa na mdhamini mkuu baada ya Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom kumaliza mkataba wake wa miaka mitatu wa kuidhamini huku ikisita kuongeza mkataba mpya japokuwa inaelezwa mazungumzo yanaendelea.

Kwa mujibu wa Ratiba ya mechi za ufunguzi inayoanza leo kwa timu za Mtibwa Sugar, Prisons, Mbeya City, African Lyon, Lipuli, Biashara United, Ruvu Shooting na Mwadui FC inaziweka kwenye wakati mgumu klabu hizo ambazo unaweza kuziathiri kwenye mechi zao za kwanza.

Ratiba leo inaonyesha Simba itaanza kutetea ubingwa na Prisons ya Mbeya wakati wageni wa Ligi Kuu, Alliance wataanza na Mbao sanjari Coastal Union ikiikaribisha Lipuli ya Iringa.

Singida itacheza na Biashara Mara huku Kagera itakuwa Kaitaba kuanza na Mwadui FC na Ruvu itapapasana na Ndanda FC.

Mbali ya kusafiri umbali mrefu kutoka kwenye mkoa mmoja kwenda mwingine kucheza mechi za ufunguzi wa ligi, pia zinalazimika kuanza kupunguza fungu la fedha kiduchu zilizopata kutoka kwa wadhamini wengine ambao ni kampuni ya Azam Media na Benki ya KCB Tanzania.

Mbaya zaidi, klabu hizo nane zitacheza mechi hizo bila kupata chochote kutokana uwepo wa kanuni ya timu mwenyeji kupata mapato yote yatokanayo na viingilio kwenye mchezo husika.

Mtibwa Sugar ambayo itaanza na Yanga, kesho Alhamisi, hadi inacheza mchezo huo imekutana na changamoto ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha.

Timu hiyo imetumia kiasi kinachokadiriwa kufikia Shilingi 7 milioni kujiandaa na mchezo huo, fedha ambazo zimegharamia safari yao ya zaidi ya Kilomita 1, 152 wakitokea jijini Mwanza lakini pia kwa ajili ya huduma za malazi, usafiri, posho na chakula kwa wachezaji wake.

Kwa maana hiyo, katika fungu la Sh 48 milioni ambazo Mtibwa watapaswa kutumia kwa miezi miwili ya awamu ya kwanza ya mgawo katika uendeshaji wa timu kiujumla, watabakiwa na Sh 41 milioni ambazo hizohizo zinatazamwa kusaidia maandalizi ya mechi zinazofuata sambamba na kulipa mishahara na posho kwa timu.

Kibarua kingine kitakuwa kwa Mbeya City ambayo itakuwa ugenini keshokutwa kuikabili Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex sawa na Biashara United nayo itaanza kuonja machungu ya gharama za Ligi Kuu kwa kuanza kwake ugenini dhidi ya Singida United.

Makadirio ya umbali kwa Prisons ni kilomita 822 na itafungua dimba na Simba kwenye Uwanja wa Uhuru leo na Sh 4 milioni na umbali wa Kilomita 586 kwa Mwadui inayocheza Kagera Sugar.

African Lyon iliyosafiri kilomita 929 hadi mkoani Shinyanga ambako itaumana na Stand United, inakadiriwa kutumia zaidi ya Sh 6 milioni, wenzao Ruvu Shooting walioko Mtwara dhidi ya Ndanda FC wametumia kiasi kinachofikia Sh 4 milioni huku wakisafiri umbali wa Kilomita 620 wakati Lipuli iko Tanga dhidi ya Coastal Union ikisafiri Kilomita 629 kutoka Iringa kwa Sh 6 mil.

Mbao na Alliance ziko nyumbaniwakati KMC kesho watakuwa wageni wa JKT Tanzania kwenye mechi yao ya ufunguzi wa Ligi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini.

Ukiondoa gharama za usafiri, malazi na chakula, changamoto kubwa kwa idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu ni fedha za kugharamia malipo ya mishahara na posho kwa benchi la ufundi, wachezaji na maofisa wa timu.