Liverpool, Barcelona zilivyoanza vibaya robo fainali Ulaya
Muktasari:
- Liverpool imekubali kipigo cha mabao 2-0 ugenini dhidi ya PSG sawa na Barcelona waliokuwa kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya Atletico Madrid.
Paris, Ufaransa. Klabu ya Liverpool imejikuta katika hali ngumu baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain (PSG) katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
PSG ambao walikuwa nyumbani walitawala mchezo huo kuanzia mwanzo hadi mwisho, wakionesha ubora mkubwa licha ya kushinda mabao mawili. Kiungo Vitinha aliongoza vyema safu ya kiungo, huku safu ya ushambuliaji iliyoundwa na Khvicha Kvaratskhelia, Ousmane Dembélé na Désiré Doué ikisumbua sana safu ya ulinzi ya Liverpool.
Bao la kwanza la PSG lilitokana na shuti la Doué lililogonga kisigino cha Ryan Gravenberch na kumpita kipa Giorgi Mamardashvili. Bao la pili lilifungwa na Kvaratskhelia baada ya kupokea pasi kutoka kwa João Neves.
Liverpool walionekana kukosa ubunifu na kujiamini, kiasi cha kushindwa kupiga hata shuti moja lililolenga lango katika kipindi cha kwanza. Juhudi zao za kurejea mchezoni zilikwama mbele ya safu imara ya ulinzi ya PSG.
Kocha Slot alifanya mabadiliko kadhaa, ikiwemo kumwacha benchi mshambuliaji nyota Mohamed Salah, jambo lililozua maswali mengi kutokana na umuhimu wa mchezo huo.
Hali ndani ya klabu hiyo inaonekana si shwari, huku kauli za nahodha Virgil van Dijk kuhusu baadhi ya wachezaji kukata tamaa zikizua mjadala mkali. Aidha, baadhi ya mashabiki wameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa timu na hata mitazamo ya baadhi ya wachezaji.
Licha ya PSG kushinda 2-0, walionekana kuwa na uwezo wa kupata mabao zaidi, huku Ousmane Dembélé akigongesha mwamba na Nuno Mendes kukosa nafasi ya wazi.
Kwa matokeo hayo, Liverpool wanakabiliwa na kazi ngumu katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Anfield. Baada ya kupindua matokeo ya bao moja dhidi ya Galatasaray katika hatua ya 16 bora, Majogoo wa Anfield watahitaji muujiza mwingine wa ili kusonga mbele jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa gumu kutokana na hali ya timu ilivyo.
Katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ilishuhudiwa Barcelona wakipoteza kwenye dimba la Camp Nou baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico Madrid.
Mabao ya Atletico yalifungwa na Julian Alvarez ambaye alifunga kwa kupiga mkwaju wa faulo jirani na eneo la hatari la Barcelona kabla ya Alexander Sorloth kuhitimisha kwa bao la pili.