Lwandamina awapigia simu wachezaji Yanga

Muktasari:

Walipopokea wakakutana na sauti nzito, ilikuwa ya kocha wao Mzambia George Lwandamina, ambaye aliwaambia maneno mafupi yaliyowapa morali kinoma.

SAA chache kutoka sasa, nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake Calvin Yondani 'Vidic'  watakuwa uwanjani kuwaongoza wenzao kusaka ushindi muhimu ili wasonge mbele hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini, wakiwa wametulia wakichezea simu zao za mkononi, ghafla bosi mmoja wa Yanga akaingia eneo walilokuwa wameketi wachezaji na kuwapa simu ili wazungumze. “Sikilizeni simu yenu hiyo”.

Walipopokea wakakutana na sauti nzito, ilikuwa ya kocha wao Mzambia George Lwandamina, ambaye aliwaambia maneno mafupi yaliyowapa morali kinoma.

Kisha Cannavaro akawasilisha ujumbe huo kwa wenzake, akisema Lwandamina amewataka kuwa majasiri uwanjani na kupambana kuhakikisha wanapata ushindi.

“Ametaka tuingie uwanjani tukiwa tumesahau matokeo ya mchezo wa awali hivyo, tutafute mabao ya haraka haraka kisha wakae na mpira na tusijaribu kucheza soka wanalotaka wapinzani wetu.”

Lakini, kingine ambacho kilionekana kuwavutia zaidi wachezaji ni taarifa kuwa, Lwandamina bado hajasaini mkataba wa kuinoa Zesco United, hivyo lolote linaweza kutokea.