Mabingwa Marekani hoi Olimpiki baada ya kutofungwa mechi 44

Thursday July 22 2021
Olimpiki pc
By AFP

Tokyo, Japan. Marekani, ambayo imetwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Olimpiki mara nne, jana Jumatano ilipata kipigo cha kwanza katika mechi 45 ilipolazwa kwa mabao 3-0 na Sweden katika mechi yao ya kwanza ya michezo hiyo jijini Tokyo.


Stina Blackstenius alifunga mabao mawili na Lina Hurtig akaongeza la tatu na kuipa Sweden, ambao walitwaa medali ya shaba mwaka 2016, mwanzo mzuri katika mechi yao ya Kundi C iliyofanyika Uwanja wa Tokyo.


Marekani, ambao watakutana na New Zealand na Australia katika mechi zao mbili za makundi zinazofuatao, ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo tangu ifungwe mabao 3-1 na Ufaransa katika mechi ya kirafiki Januari mwaka 2019.


"Tulibanwa," alisema mshambuliaji wa Marekani, Megan Rapinoe. "Nilidhani tulikuwa na wasiwasi kidogo, tulibanwa kidogo, kufanya mambo mabaya."


Hicho ni kipigo cha pili ndani ya dakika tisini kwa Marekani katika Michezo ya Olimpiki. Walifungwa katika mechi yao ya kwanza ya michezo ya mwaka 2008 lakini wakaishia kutwaa medali ya dhahabu jijini Beijing.


"Ni dhahiri tunajiweka kwenye shimo kubwa, lakini ni sisi pekee tunaoweza kujiondoa humo ndani," alisema kocha wa Marekani, Vlatko Andonovski.

Advertisement


"Haitakuwa rahisi. Hatuna budi kupata matokeo mazuri katika mechi mbili zijazo, lakini ukweli kwamba bado kuna nafasi, najua timu hii haitakata tamaa."


Kocha wa Sweden, Peter Gerhardsson alionya wachezaji wake kutojiamini kupita kiasi baada ya kiwango hicho kizuri.
"Ndio, katika hali ya kawaida (hilo linawezekana), lakini pia tunajua kuwa tunaweza kufurahia pointi tatu," alisema.


"Lakini ni mashindano marefu. Mechi sita katika siku 17 kama utafika mwisho. Hatujafika robo fainali bado, kwa hiyo ni lazima tupate matokeo mazuri zaidi katika kila mechi."
Sweden ilifuta matumaini ya Brazil katika michezo ya Rio de Janeiro miaka mitano iliyopita baada ya kushinda kwa mikwaju ya penati.

Advertisement