Madaktari watoa sababu za kifo cha uwanjani

Muktasari:
Mbali ya sababu hizo za kimwili pia Dk Mngazija alitaja sababu zinazochangiwa na mamlaka za soka na klabu kushindwa kupima afya za wanamichezo wao.
Dar/ Mwanza. Matukio ya kuanguka na kufa ghafla kwa wanamichezo siyo geni duniani. Zipo sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa za kutokea kwa matukio hayo ya kusikitisha.
Miongoni mwa wanamichezo walioanguka na kufa ni kiungo wa Cameroon, Marc Vivien Foe mwaka 2003, alipokuwa akiichezea timu yake dhidi ya Colombia, pia, Patrick Ekeng aliyefariki dunia Mei 6, 2016. Yeye alidondoka wakati wa mechi dhidi ya FC Viitorul Constanța, ikiwa ni dakika saba baada ya kuingia akitokea benchi alikimbizwa hospitali alikofia saa mbili baadaye.
Vifo hivyo vimezua mijadala mingi kwa wasomi, wataalamu wa tiba za wanamichezo. Nchini, Dk Shecky Mngazija alisema jana kuwa kifo kama kile chipukizi wa Mbao FC ya Mwanza, Ismail Halfan juzi kinaweza kusababishwa na sababu kuu mbili.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Dk Mngazija alisema vifo cha ghafla ni matukio yanayowakumba wanamichezo, yanayoumiza kutokana na sababu mbalimbali. “Kifo cha aina hiyo kinawezekana kusababishwa na mapafu au moyo ulishindwa kufanya kazi. Pia, inawezekana hewa ya oksijeni haikufika kwenye ubongo au hata ini au figo zilishindwa kufanya kazi kutokana na presha ya mwili,”alisema Mngazija na kuongeza kuwa wataalamu waliofanyia uchunguzi mwili wa mchezaji huyo ndio watatoa majibu sahihi.
Mbali ya sababu hizo za kimwili pia Dk Mngazija alitaja sababu zinazochangiwa na mamlaka za soka na klabu kushindwa kupima afya za wanamichezo wao.
“Timu kukosa wataalamu wa kuwashawishi kupima afya za wachezaji. Pili, viongozi wengi wa klabu wanakwepa gharama na tatu wachezaji wanakwepa kutokana na kuhofia matokeo ya vipimo,” alisema Mngazija ambaye ni naibu katibu mkuu wa Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo Tanzania (Tasma).
Chipukizi huyo alipoteza maisha wakati akiitumikia timu yake katika mchezo wa ligi ya vijana dhidi ya Mwadui uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Sababu zaidi za vifo vya ghafla
Wakielezea kitaalamu vyanzo vya vifo vya ghafla vinavyotokea uwanjani, kwa nyakati tofauti jana, Dk Samwel Shita na Juma Sufian walisema vinasababishwa na tatizo la moyo.
“Ingawa hakuna taarifa rasmi ya ‘postmortem’ (uchunguzi), lakini kwa namna ilivyotokea tatizo hilo uwa linasababishwa na ugonjwa ujulikanao kama kuongezeka kwa nyama za chumba cha kushoto cha chini cha moyo.” alisema Dk Juma Sufian aliyewahi kuwa daktari wa Yanga.
Alisema tatizo hili uwakumba wanamichezo wenye umri chini ya miaka 35 na chanzo cha kuvimba kwa nyama hizo halijajulikana.
“Mchezaji anakuwa hajijui hivyo kinachotokea mwili unakuwa unahitaji oksijeni ya kutosha hivyo inabidi damu izunguke kwa nguvu na moyo unasukuma damu nyingi hali inayosababisha vifo vya ghafla,” alisema.
Dk Shita, ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya michezo alisema vifo vya ghafla husababishwa na matatizo ya moyo ambayo hayajulikani vizuri.
“Unapocheza, moyo unafanya kazi kwa kiasi kikubwa, kama moyo wako ulishakuwa dhaifu, pamoja na kusukuma damu lakini pia moyo ina mishipa yake hivyo ikitokea ikashindwa ku pampu inapelekea vifo vya ghafla.
“Kingine, ni umeme wa moyo kuwa shida, hali inayosababisha mapigo ya moyo kutokuwa vizuri na kusababisha vifo,” alisema Dk Shita.
Wakati Dk Mngazija akitoa sababu hizo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Thomas Rutta alithibitisha kupokea maiti ya mchezaji huyo, lakini akakataa kuzungumzia chanzo cha kifo hicho, akitaka waulizwe watu wa Jeshi la Polisi.
“Nadhani umwasiliane na polisi, ndio watatoa maelezo zaidi, maadili ya utumishi wa umma, sisi hatuhusiki,” alisema Dk Rutta.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema bado uchunguzi wa kifo cha mchezaji huyo unaendelea watatoa taarifa rasmi baada ya kukamilika.
Kauli za wadau
Vilio na simanzi vimetawala jiji la Mwanza baada ya kifo cha mshambuliaji huyo wadau, wazazi na viongozi wa timu hiyo wakielezea walivyoguswa na kifo hicho.
Mwenyekiti wa Mbao FC, Sory Njashi alisema tukio hilo ni la kipekee ambalo kamwe halitasahaulika kwani imekuwa pigo kwao.
“Ni pigo kwa kweli, tulimtegemea sana, lakini ndiyo hivyo tena. Hatutasahau,” alisema Njashi kwa masikitiko.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Masoud alisema mchezaji huyo afya yake ilikuwa salama na alikuwa mchangamfu kama siku nyingine, hakuonyesha kuwa na ugonjwa wowote.
“Sisi tumeshangaa, yaani alianguka chini tukaenda kumwangalia, tunamuweka chini alikuwa tayari amekufa, hadi chanzo hakijajulikana,” alisema Masoud.
Babu wa mchezaji huyo, Hamidu Suleiman alisema kuwa kifo hicho kimewashtua wanafamilia na kwamba hawatoweza kusahau milele. “Yaani, sijui niseme nini, kwa kweli tumeshtushwa na taarifa hii ambayo sidhani kama itakuja sahaulika vichwani mwetu…Kijana alikuwa na afya nzuri, msikivu na hata mwenye upendo, hatujui nini sababu ya kifo chake,” alisema Suleiman.
Kocha Osuri Kosuri aliyekuwa na mchezaji huyo katika kikosi cha timu ya Kanda ya Ziwa kwenye michezo ya Umisseta (shule za sekondari) alisema, juzi alimtumia ujumbe wa kumtaka ampigie simu.
“Nilipoongea naye aliniambia wanajiandaa na mechi yao na Mwadui, nikamwambia apambane na alikuwa mchangamfu nilishtuka nilipoambiwa amekufa,” alisema Kosuri.
Hata hivyo Kosuri alitoa angalizo kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF)kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya huduma ya kwanza uwanjani, ikiwapo oksijeni ambayo haikuwepo uwanjani hapo pamoja na gari la wagonjwa.
“Ili liwe fundisho kwetu kwani hakukuwa na huduma yoyote nzuri ya kwanza na ukiangalia hata gari la wagonjwa halikuwapo mchezaji alibebwa kwenye gari la Zimamoto,” alisema Kosuri.
Mshambuliaji wa Toto Africans, Baraka Mitego alisema walikuwepo uwanjani wakati tukio hilo linatokeaa, kamwe hatoweza kulisahau.
“Imeniuma, ni kijana mwenzetu nilikuwapo uwanjani wakati anadondoka kwa kweli imeniuma, ila ndiyo kazi ya Mungu,” alisema.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Nassib Mabrouk alisema kuwa taarifa hizo ni pigo kwa tasnia ya mpira kwa Mwanza
“Ni msiba mkubwa kwetu ila ni kazi ya Mungu. Sisi MZFA tunatoa pole nyingi kwa uongozi wa Mbao na wazazi wa marehemu kwa msiba uliowapata,” alisema Mabrouk.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Fredrick Nwaka (Dar ), Saddam Sadick na Masoud Masasi (Mwanza)