Madrid yapata ushindi wa kwanza, Wydad ikitupwa nje
Muktasari:
- Wydad sasa imeondoshwa rasmi kwenye mashindano hayo kwani katika michezo miwili iliyocheza imeambulia vipigo.
Charlotte, Marekani. Real Madrid imeibuka na ushindi wa kwanza katika mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu baada ya kuichapa Pachuca ya Mexico mabao 3-1 katika mchezo wa kundi H, uliopigwa kwenye Uwanja wa Bank of America, Charlotte, Marekani.
Hata hivyo, ushindi huo wa mabingwa hao wa kihistoria wa Ulaya umekuja katika mazingira magumu baada ya kujikuta wakicheza pungufu kwa muda mrefu kufuatia mchezaji wao Raúl Asencio kutolewa kwa kadi nyekundu mapema katika dakika ya saba.
Licha ya upungufu huo, kikosi cha Madrid chini ya kocha Xabi Alonso kilionyesha uimara na nidhamu ya hali ya juu uwanjani, huku Jude Bellingham akifungua pazia la mabao dakika ya 35 akimalizia pasi ya Arda Güler.
Madrid iliendelea kufanya mashambulizi kwa wapinzani wao na kuongeza bao la pili kupitia kwa Arder Güler kabla ya mapumziko, mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika Madrid ilitoka kifua mbele.
Madrid walirejea kwa kasi ileile katika kipindi cha pili mpaka ilipofika dakika ya 66 ambapo Federico Valverde alifunga bao la tatu kwa shuti kali kabla ya Pachuca kupata bao la kufutia machozi dakika ya 80 kupitia kwa Elias Montiel, baada ya mpira wake kugonga mguu wa Tchouaméni na kumchanganya kipa, Thibas Courtois.
Kipa huyo wa Madrid ndiye alikuwa nyota wa mchezo kwa kuokoa michomo kadhaa hatari, hasa kipindi cha pili ambapo Pachuca walitumia nafasi ya kusaka mabao ya kusawazisha, bila mafanikio.
Ushindi huo unaifanya Real Madrid kufikisha pointi nne baada ya michezo miwili na kujikita kileleni mwa Kundi H, wakisubiri pambano lao la mwisho dhidi ya Salzburg kuhakikisha nafasi ya kutinga hatua ya mtoano.
Kwa upande wa Pachuca, matokeo hayo yamewafanya kubaki mkiani bila alama na sasa wanasubiri pambano la mwisho dhidi ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Juventus yaiondosha Wydad Casablanca
Juventus imeendelea na kasi kubwa katika Kundi G la Kombe la Dunia la Klabu baada ya kuikandamiza Wydad Casablanca kwa mabao 4‑1 katika mchezo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Lincoln Financial Field, Philadelphia.
Katika mchezo huo Juventus ilipata bao la mapema katika dakika ya sita baada ya beki wa Wydad, Boutouil kujifunga. Bao la pili lilifungwa na Yildiz ambaye aliachia shuti kali nje ya boksi lililomshinda kipa wa Wydad katika dakika ya 16.
Wydad ilirejesha matumaini katika dakika ya 25 kupitia kwa Thembinkosi Lorch aliyemalizia pasi safi ya Nordin Amrabat na kuipeleka mapumziko ikiwa na matumaini ya kurudi mchezoni katika kipindi cha pili.
Hata hivyo, Juventus iliendelea kufanya mashambulizi kwenye lango la Wydad ambapo Yildiz alifunga bao la tatu katika dakika ya 69 baada ya kupokezana pasi na Randal Kolo Muani, huku Dusan Vlahović akihitimisha karamu ya mabao kwa mkwaju wa penalti katika muda wa nyongeza na kupeleka kichapo cha mabao 4-1.
Baada ya kipigo hicho Wydad sasa imeondoshwa rasmi kwenye mashindano hayo kwani katika michezo miwili iliyocheza imeambulia vipigo ikiwa katika nafasi ya tatu bila pointi kwenye kundi G sawa na Al Ain ambayo nayo haina pointi baada ya kuruhusu kipigo kingine jana cha mabao 6-0 dhidi ya Manchester City.