Makata anukia Polisi Tanzania

ALIYEKUWA Kocha wa Mbeya Kwanza, Mbwana Makata yupo mbioni kujiunga na Polisi Tanzania ili kwenda kurithi mikoba ya Mrundi Joslin Bipfubusa.

Polisi Tanzania iliachana na Joslin aliyechukuwa mikoba ya Malale Hamsini baada ya kutofurahishwa na matokeo ambayo timu ilikuwa ikiendelea kuyapata.

Habari kutoka kwa kigogo wa juu wa timu hiyo, ilieleza kuwa walipokea wasifu mbalimbali wa makocha wakihitaji kuifundisha timu yao kipindi hiki lakini kwasasa wanahitaji kocha ambaye atawavusha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Tulipokea CV (wasifu) kutoka kwa makocha mbalimbali lakini kwasasa tunayempa kipaumbele kikubwa ni Makata kwa sababu ana uzoefu wa Ligi ya hapa nyumbani,” alisema kigogo huyo.

Kiongozi huyo alisema lengo la kwanza ni kuwatoa sehemu waliopo kwani hadi sasa wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi tisa wakicheza mechi 12.

Makata anatajwa kurejea Ligi Kuu baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa ligi baada ya kudaiwa kuamuru wachezaji wa Mbeya Kwanza kugomea mchezo wao wa Ligi dhidi ya Namungo FC.