Mambo manne yaliyojitokeza robo fainali Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

  • Baada ya mechi za marudiano za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kumalizika jana Jumatano, mambo manne yamejitokeza.

Paris, Ufaransa (AFP). Baada ya mechi za marudiano za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kumalizika jana Jumatano, mambo manne yamejitokeza.


Inaonekana Zinedine Zidane ana nafasi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya nne, akiwa kocha baada ya Real Madrid kuiondoa Liverpool, Paris Saint Germain inaelekea kuondoa mwiko barani Ulaya baada ya kuwavua ubingwa Bayern Munich, huku Jude Bellingham wa Dortmund akionekana kufuata nyayo za Jadel Sancho na vijana wapya wa Chelsea wakiendelea kufanya maajabu.


Zidane kupewa nafasi ya kuwa kocha pekee aliyetwaa ubingwa wa Ulaya mara nne ndicho kitu ambacho Real Madrid ilionekana kuwa nacho wakati ilipokutana na Liverpool jana Jumatano.


Kwa sasa Zidane analingana na makocha wengine wawili kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa/vikombe vya Ulaya mara tatu, akiwa pamoja na Carlo Ancelotti na kocha wa zamani wa Liverpool, Bob Paisley, baada ya Mfaransa huyo kutwaa ubingwa huo mara tatu mfululizo katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya kwanza kama kocha wa vigogo hao wa Madrid.


Kwa mara nyingine, Madrid itakuwa ikipewa nafasi ya kufika fainali wakati itakapokutana na Chelsea katika nusu fainali na hivyo kupata nafasi ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya 14.


Jana Jumatano, timu yake haikuwa katika ubora uliotumika kuisambaratisha Liverpool kwa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza, lakini mchanganyiko wa uzuiaji wa kijasiri pamoja na umaliziaji mbovu wa wenyeji ulimaanisha mabingwa hao wa Hispania hawakuwa hatarini kuondolewa.

Hatimaye PSG yakaribia mafanikio Ulaya?
Paris Saint-Germain ilipata mafanikio makubwa kuwahi kutokea katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumanne wakati ilipofuzu kucheza nusu fainali kwa kuiondoa Bayern Munich kwa sheria ya bao la ugenini, na bila shaka timu hiyo iliyofika fainali msimu uliopita, itataka ipate mafanikio zaidi mwaka huu.


"Tunahitaji hilo. Tulitaka kuonyesha kuwa tunaweza kuwashinda, na tulifanya hivyo," alisema Neymar, ambaye aling'ara katika mechi zote mbili kali zilizoisha kwa sare ya jumla ya mabao 3-3.


Kasi kali ya PSG katika mashambulizi ya kushtukiza iliiwezesha kupata ushindi wa ugenini katika mechi za kwanza za hatua ya mtoano dhidi ya Barcelona na Bayern.


Kwa jinsi timu hiyo ilivyoshikamana na kuziondoa timu vigogo barani Ulaya, ni wazi kocha Mauricio Pochettino ana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ulaya baada ya kushindwa kufanya hivyo akiwa na Tottenham mwaka 2019.


Kutawala bara la Ulaya itakuwa ni hitimisho la jitihada kubwa zilizofanywa katika kipindi cha miaka kumi kwa wamiliki matajiri wa PSG kutoka Qatar, ambao wanategemea kuwabakiza washambuliaji nyota Neymar na Kylian Mbappe.


"Ni dhahiri kwamba najisikia vizuri sana hapa Paris Saint-Germain. Najisikia furaha kuliko ilivyokuwa awali," Neymar aliiambia chaneli ya Brazil ya TNT Sports baada ya kuiwezesha timu hiyo kupata nafasi ya kucheza na Manchester City ambayo pia inamilikiwa na matajiri wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Bellingham afuata nyayo za Sancho
Jude Bellingham alitangaza kuingia kwake katika hatua kubwa ya michuano ya Ulaya licha ya Borussia Dortmund kuondolewa na Manchester City, kwa kung'ara katika mechi ya jana.


Akiwa na miaka 17 na siku 289, Bellingham amekuwa mchezaji wa pili mdogo kufunga katika hatua ya mtoano ya historia ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Alichukua mpira nje ya eneo la penati na kupiga kiki iliyopinda wakati ikijaa wavuni na kufanya matokeo kuwa sare ya mabao  2-2 na hivyo Wajerumani kuwa mbele kwa sheria ya bao la ugenini.


Bao hilo halikuitosha Dortmund kuingia nusu fainali-- ambako ingekutana na PSG-- kwa kuwa penati iliyopigwa na Riyad Mahrez katika dakika ya 10 ya kipindi cha pili na bao la Phil Foden liliwahakikishia vijana wa Pep Guardiola tiketi ya kusonga mbele.


Lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa England, ambaye alisajiliwa Dortmund akitoka klabu ya daraja la kwanza ya Birmingham City kwa dola 30 milioni za Kimarekani mwaka jana, aliongezea mafanikio ya kufunga bao lake la kwanza Ligi Kuu ya Ujerumani mwishoni mwa wiki, kwa kumfunika Erland Braut Haaland, aliyecheza chini ya kiwango jana.


Bellingham anaonekana kuwa anafuata nyayo za kuelekea kuwa nyota za mchezaji mwenzake wa Dortmund, Jadon Sancho, ambaye aliibukia katika timu ya vijana ya City na sasa ni mmoja wa wachezaji wachezaji wenye kipaji wanaosakwa barani Ulaya.

Vijana ngangari Chelsea kufanya maajabu
Kocha Thomas Tuchel anaonekana kuwa katika hali nzuri baada ya Chelsea kuiondoa Porto kwa njia ambayo ni ya kiweledi iliyokuwa ndani ya timu yake iliyojaa vijana.


Porto ilikuwa imemuondoa Cristiano Ronaldo na Juventus yake katika raundi iliyotangulia kwa kujilinda vizuri katika mechi zote mbili, lakini walikuwa ni Chelsea walionyesha nidhamu inayotakiwa katika hatua ya robo fainali na hivyo kuwaondoa Wareno hao.


Ulikuwa ni ushindi uliotokana na kuwachezesha wachezaji wapya katika Ligi ya Mabingwa kama Mason Mount, Reece James, Kai Havertz, Ben Chilwell na Christian Pulisic.


"Mason alifunga bao lake la kwanza katika mashindano haya katika mechi ya kwanza. Mbappe anapofunga au (Mohamed) Salah anapofunga au (Karim) Benzema anapofunga, inakuwa ni bao la 100 au mabao yao ya 50 katika mashindano," alisema Tuchel.


"Ukiwa pale tu, unacheza ili kufika fainali. Tunahitaji kila dakika kujifunza na kukua. Huwezi kuwa bora zaidi bila ya uzoefu huu."