Prime
Mambo manne yanayomsubiri Kocha mpya Simba
Muktasari:
- Rekodi zinaonyesha, Simba hii ni mara ya saba inacheza hatua ya makundi michuano ya CAF, mara zote ilizowahi kucheza hatua hiyo imefanikiwa kuvuka kwenda robo fainali, haijawahi kukwama kama ilivyo kwa wawakilishi wengine wa Tanzania waliowahi kucheza makundi.
Dar es Salaam. Simba baada ya kuachana na Dimitar Pantev Desemba 2, 2025, sasa ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya wa kuja kuinoa timu hiyo.
Wakati mchakato huo ukiendelea, Seleman Matola amekabidhiwa kikosi akiongoze. Tayari Matola ameiongoza Simba kucheza mechi mbili za ligi dhidi ya Mbeya City na Azam.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia namna mchakato wa kumsaka kocha mpya unavyoendelea.
Ally amesema: "Maombi ni mengi kwelikweli kutoka kwa mawakala na makocha wenyewe. Kila mmoja kwa nafasi yake anaomba kuja kuifundisha Simba.
"Wapo makocha ambao wana timu wanazifundisha hapa Afrika na Ulaya, wengine hawana kazi. Wote hawa wanatuma maombi.
"Mipango yetu ipo hivi, baada ya mechi dhidi ya Azam, timu itakwenda mapumziko kidogo, baada ya hapo tutarejea kwa ajili ya maandalizi mechi zijazo za CAF.
"Tutakaporejea kuendelea na maandalizi ya mechi zetu kuanzia Januari 23 mwakani tuwe tushapata kocha tayari. Yaani tumpe mwalimu kama pre-seasom fulani hivi ya wiki tatu nne ili awajue wachezaji. Tutakapoanza mechi za mashindano awe tayari familia na kikosi chake."
Simba inapoendelea kusaka kocha mpya, kuna mitihani minne inamkabili mrithi huyo wa Pantev ambayo Mwananchi inakuchambulia.
Kufuzu robo fainali CAF
Rekodi zinaonyesha, Simba hii ni mara ya saba inacheza hatua ya makundi michuano ya CAF, mara zote ilizowahi kucheza hatua hiyo imefanikiwa kuvuka kwenda robo fainali, haijawahi kukwama kama ilivyo kwa wawakilishi wengine wa Tanzania waliowahi kucheza makundi.
Kuanza vibaya kwa Simba msimu huu ikipoteza mechi mbili za kwanza, kocha ajaye anapaswa kubadilisha matokeo hayo na kuleta ushindi utakaoivusha kwenda robo fainali na kulinda rekodi yao.
Katika mtihani huo, Simba inapaswa kupambana kuifunga Esperance ugenini na nyumbani, mechi hizo mbili ndizo zinazofuata baada ya michuano kusimama kupisha AFCON 2025.
Januari 23, 2026, Simba itakuwa Tunisia kucheza dhidi ya Esperance, kisha Januari 30, 2026, timu hizo zitakutana tena Dar es Salam.
Ulazima wa Simba kushinda mechi hizi unatokana na kwamba hivi sasa haina pointi, hivyo inapaswa kuzikusanya hizo sita au hata nne kuweka mazingira vizuri ikizingatiwa vinara wa kundi lao la D, Petro Atletico na Stade Malien, pia wanakutana wenyewe kila mmoja akiwa na pointi nne.
Esperance yenye pointi mbili, nayo inazipigia hesabu mechi hizo mbili, hivyo haitakuwa rahisi.
Kushinda mataji
Kwa misimu minne mfululizo, Simba inapitia maumivu ya kukosa mataji mawili makubwa hapa nchini. Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Wakati Simba ikiwa kwenye maumivu hayo, watani zao wa jadi Yanga ni kicheko kwani muda huo imetawala kwa kuyabeba mataji yote hayo.
Mara ya mwisho Simba kubeba taji la Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu wa 2020-2021 ilipokuwa ikifundishwa na Kocha Didier Gomes. Msimu huo pia ilikuwa mara ya mwisho kubeba Kombe la FA.
Baada ya hapo, wamepita makocha wa kigeni sita bila ya mataji hayo ambao ni Pablo Franco, Zoran Maki, Roberto Oliveira 'Robertinho', Abdelhak Benchikha, Fadlu Davids na Dimitar Pantev.
Ukiweka kando mataji hayo, Robertinho alipambana akashinda Ngao ya Jamii mwaka 2023 akiichapa Yanga. Hata hivyo, Yanga hiyohiyo ilichangia kuondoka kwake alipopokea kichapo cha mabao 5-1, Novemba 6, 2023.
Kupandisha viwango vya wachezaji
Kuna kinachoendelea ndani ya kikosi cha Simba hivi sasa ikionekana mastaa wa timu hiyo viwango vimeshuka.
Hilo limejidhihirisha katika mashindano ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika tangu hatua za mwanzoni hadi sasa timu ikiwa makundi.
Licha ya Simba kupenya hatua za awali na kufuzu makundi, lakini kitendo cha kutoshinda mechi yoyote nyumbani ni dhahiri kuna tatizo.
Simba ilianza kuichapa Gaborone United 1-0 ugenini, nyumbani matokeo yakawa 1-1. Kisha ikaenda ugenini kuichapa Nsingizini Hotspur 3-0, ikarudi nyumbani ikaambulia 0-0.
Hatua ya makundi, imepoteza mechi zote mbili na kuburuza mkia Kundi D linaloongozwa na Petro Atletico yenye pointi nne sawa na Stade Malien wakati Esperance ikiwa nazo mbili. Simba haina kitu.
Mchezaji kama Jean Charles Ahoua ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akipachika mabao 16 na asisti tisa, msimu huu katika ligi ana bao moja na asisti moja akicheza mechi nne.
Kimataifa msimu uliopita wakati Simba inacheza fainali Kombe la Shirikisho, Ahoua alifunga mabao matatu, yote yalipatikana kuanzia hatua ya makundi hadi fainali. Msimu huu hadi sasa hajafunga.
Mbali na Ahoua, Elie Mpanzu na Steven Mukwala wanaocheza eneo la ushambuliaji nao wanaonekana kutokuwa makini, nafasi nyingi zinatengenezwa, lakini wanashindwa kuzigeuza kuwa mabao. Kocha mpya ana kazi ya kuboresha viwango vyao na mastaa wote kikosini hapo.
Kuifunga Yanga
Machi 1, 2026 imepangwa kupigwa Dabi ya Kariakoo, Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Hii ni dabi ya kwanza kwa timu hizo kwenye ligi msimu huu baada ya awali iliyopangwa kuchezwa Desemba 13, 2025 kusogezwa mbele.
Simba imekuwa ikiteseka kusaka ushindi mbele ya Yanga kwa muda mrefu kiasi cha kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kukosa amani.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa Agosti 13, 2023 katika Ngao ya Jamii iliposhinda 3-1 kwa penalti baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.
Tangu hapo, timu hizo zimekutana mara sita katika mashindano tofauti na Yanga imeshinda zote mfululizo.
Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Simba 1-5 Yanga (Novemba 5, 2023), Yanga 2-1 (Aprili 20, 2024), Yanga 1-0 Simba (Agosti 8, 2024), Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19, 2024), Yanga 2-0 Simba (Juni 25, 2025) na Yanga 1-0 Simba (Septemba 16, 2025).