Man City yapewa onyo kali

Muktasari:
- Matajiri hawa wa Jiji la Manchester hapo awali walihukumiwa na mamlaka za soka nchini England Februari 2023 lakini ilikata rufaa na kupinga mashtaka yao.
MANCHESTER, ENGLAND. Mchezaji wa zamani wa Aston Villa na Wolves ambaye kwa sasa ni mchambuzi, Andy Gray amesema Manchester City inaweza ikapokonywa pointi kibao kutokana na mashtaka 115 ya kukiuka sheria za matumizi ya pesa yanayoikabili.
Matajiri hawa wa Jiji la Manchester hapo awali walihukumiwa na mamlaka za soka nchini England Februari 2023 lakini ilikata rufaa na kupinga mashtaka yao.
Kesi zinazowakabili zinatarajiwa kusikilizwa mwisho wa mwaka huu na wachambuzi wanadai kuna uwezekano mkubwa wababe hao wakakutwa na kitu kizito.
Kukatwa pointi ama kushushwa daraja ni kati ya adhabu wanazoweza kupata ikiwa watakutwa na hatia na Gray ambaye alifanya mahojiano na BeIn Sports anaamini kukatwa pointi nyingi ndio adhabu yenye asilimia kubwa kwa vigogo hao.
"Nini kitatokea? Nafikiria ingawa sina uhakika wanaweza kunyang'anywa pointi nyingi, naamini watapatikana na hatia tu, huwezi ukawa na mashtaka 115 na yote yasikuingize hatiani, nadhani sote tunafahamu kama kusingekuwa na ushahidi ambao unaweza kuwaingiza kwenye hatia wasingefunguliwa mashtaka lakini ushahidi upo," alisema Gray.
"Sidhani kama watawanyang'anywa mataji, hivyo kinyume chake wanaweza kunyang'anywa pointi ama kutozwa faini ingawa sioni kama hilo litafanyika kwa sababu wanaweza kuilipa na haitowapa maumivu ingawa mamlaka pia zinaweza kuwapiga faini na kuwakata pointi pia."
Kocha wa Man City, Pep Guardiola alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema ana furaha kwa sababu inaenda kusikilizwa hivi karibuni na akaongeza kwamba hiyo haiathiri utendaji wa timu yake kwani mambo hayo yamekuwa yakiwaandama kwa mwaka wanne sasa.