Mancini aula Italia

Muktasari:

  • Uteuzi wa Mancini unamaliza sintofahamu ya miezi sita juu ya nani hasa angepewa kibarua cha kurudisha heshima ya Italia iliyoshindwa kufuzu Kombe la Dunia chini ya Ventura aliyetimuliwa Novemba. Italia ilishiriki mfululizo kwa miaka 60 tangu mwaka 1958 .

Kocha wa zamani wa Inter Milan na Manchester City, Roberto Mancini anakabiliana na kibarua kizito cha kuirudisha timu ya Taifa ya Italia ‘Azzuri’ kwenye mstari baada ya juzi kutangazwa kama kocha mkuu akirithi mikoba ya Gian Piero Ventura aliyeshindwa kuiongoza timu hiyo kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Urusi mwezi ujao.

Uteuzi wa Mancini unamaliza sintofahamu ya miezi sita juu ya nani hasa angepewa kibarua cha kurudisha heshima ya Italia iliyoshindwa kufuzu Kombe la Dunia chini ya Ventura aliyetimuliwa Novemba. Italia ilishiriki mfululizo kwa miaka 60 tangu mwaka 1958 .

Majina kadhaa yalikuwa yakitajwa kupewa jukumu hilo, miongoni mwao akiwemo Mancini mwenyewe, kocha wa Chelsea, Antonio Conte pamoja na Carlo Ancelloti ambaye kwa sasa hana timu.

Kibarua cha kwanza kwa Mancini, ambaye kabla ya kupewa jukumu hilo alikuwa akiinoa timu ya Zenith St. Petersburg ya Urusi, ni kuhakikisha Italia inafuzu kwenye mashindano ya Ulaya mwaka 2020.

Mancini ni miongoni mwa makocha wanaoheshimika nchini Italia kutokana na mafanikio aliyopata katika klabu mbalimbali alizoziongoza ikiwa ni pamoja na kutwaa Kombe la Coppa Italia akiwa na Fiorentina mwaka 2001, kuiongoza Inter Milan kutwaa Ubingwa wa Italia kwa misimu mitatu mfululizo pamoja na kutwaa taji la Ligi Kuu England na Kombe la FA England akiwa na Manchester City.