Manula awakimbiza makipa wa Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Katika mechi sita za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili na inashika nafasi ya pili katika chati ya timu ambazo hazijaruhusu idadi kubwa ya mabao katika hatua hiyo.

Kitendo cha kucheza mechi nne bila kuruhusu bao kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kimemfanya Aishi Manula awapige bao makipa wanne waliowahi kushirki Fainali za Kombe la Dunia kwa nyakati tofauti katika chati ya walinda mlango waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao.

Makipa hao ambao Manula amewaacha kwenye mitaa ni Farouk Ben Mustapha wa Esperance ya Tunisia, Daniel Akpeyi na Itumeleng Khune wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini pamoja na kipa wa Al Ahly ya Misri, Mohamed El Shenawy.

Ben Mustapha ambaye alikuwa kipa chagua la kwanza la Tunisia katika Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika huko Russia mwaka 2018, amecheza bila kuruhusu nyavu zake kuguswa katikamechi moja tu kati ya tano alizokuwemo katika kikosi cha Esperance kwenye hatua ya makundi.

Kipa aliyeidakia Afrika Kusini katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Itumeleng Khune, yeye katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu amecheza jumla ya mechi tatu na kati ya hizo, ni moja tu ambayo hakuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Daniel Akpeyi aliyecheza mechi mbili bila kuruhusu bao kati ya tatu za Kaizer Chiefs kwenye hatua ya makundi, yeye alikuwemo katika kikosi cha Nigeria kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 na zile za mwaka 2018.

Nahodha wa Al Ahly, Mohamed El Shenawy ambaye alisimama langoni wakati Misri inashiriki Kombe la Dunia mwaka 2018, yeye hajaruhusu bao katika mechi tatu kati ya sita alizoidakia timu yake katika hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Lakini sio tu makipa hao wanne pekeewaliokimbizwa na manula bali mwingine ni kipa wa Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Uganda, Denis Onyango ambaye anatajwa kama mmoja wa makipa bora Afrika kwa sasa ambaye yeye amecheza mechi mbili tu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa kati ya nne alizokuwemo katika kikosi cha kwanza cha timu yake.

Kiujumla Manula anashika nafasi ya nne katika chati ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Ahmed Reda Tagnanout wa Wydad Casablanca anaongoza chati hiyo akiwa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi zote tano alizoidakia timu hiyo ya Morocco katika hatua ya makundi akifuatiwa na Moussa Camara wa Horoya ya Guinea ambaye yeye katika mechi tano alizocheza, nyavu zake hazijatikiswa mara nne.

Kipa wa CR Belouizdad ya Algeria, Toufik Moussaoui anashika nafasi ya tatu kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambapo katika mechi nne alizoidakia timu hiyo, mechi tatu alimaliza bila nyavu zake kuguswa.

Ali Achrine wa Al Hilal ya Sudan anashika nafasi ya tano kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambapo katika mechi tano alizoichezea timu yake, nyavu zake hazijaguswa mara tatu.