Manzoki anakuja Dar, Simba kuanza usajili leo

Dirisha dogo la usajili limefunguliwa leo Desemba 15, mabosi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na benchi la ufundi chini ya Kocha Juma Mgunda watafanya kikao kizito kuhusu hatma ya usajili, huku Cesar Manzoki akitarajiwa kutua nchini.

Mpango wa Simba kumpata straika wa Dalian Professional FC ya China, Manzoki huenda ukapotea kutokana na mkwanja anaopata mshambuliaji huyo.

Kabla ya kujiunga na Dalian, Manzoki alikuwa amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba uliyotakiwa kuanza mwanzo wa msimu huu ila ilikuwa ngumu kumpata kutokana na timu yake ya wakati huo, Vipers ya Uganda kudai bado ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi.

Kutokana na ugumu huo wa kumpata Manzoki kwa wakati huo mabosi wa Simba wakishirikiana na watu wao wa karibu, Dilian walishirikiana kukamilisha dili la kwenda kuipigania klabu hiyo na walifanikiwa.

Manzoki alisaini mkataba wa miezi sita aliokuwa akichukua zaidi ya Sh20 milioni kwa mwezi kama mshahara wake huku akichukua mkwanja mwingine mrefu kama thamani ya usajili.

Mkataba wa Manzoki unamalizika mwezi Desemba na uongozi wa Simba uliamini utakamilisha mpango wa kumpata straika huyo mwenye asili ya DR Congo, ili kuja kuongeza makali mzunguko wa pili na Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa hatua ya makundi.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza huenda wakashindwana kukamilisha dili la Manzoki kukupiga kwenye klabu yao kutokana na timu yake ya sasa, Dilian kuvutiwa na huduma yake.

Mabosi wa Dilian tayari wamefanya mazungumzo na Manzoki na kukubaliana kumpa mkataba mwingine wenye thamani kubwa na mshahara ambao utakuwa mrefu zaidi ya ule wa awali.

Inaelezwa mshahara wa Manzoki kwenye mkataba wake mpya huko China anaweza kuvuta zaidi ya Sh40 milioni kwa mwezi kama mshahara na ile hela ya kusaini mkataba ni zaidi ya Simba iliyokuwa tayari kumpatia.

Kutokana na Manzoki kuwa na uhakika wa kusaini mkataba mpya huko China, chanzo kinasema atakuja nchini mwezi huu kufanya kikao na Try Again ili kumueleza masilahi makubwa anayopata huko.

“Atakuja Tanzania kwa ajili ya kumshukuru Try Again kwa juhudi na uaminifu aliouonyesha, nafikiri atakuja mwezi huu baada ya hapo atarudi kwenye timu yake, huyu jamaa ni mtu muungwana sana,” kilisema chanzo.

Manzoki atamshukuru ‘Try Again’ kwa jitihada alizofanya hadi kumpa mkataba wa miaka miwili na kupambana kumtoa Vipers ila hataweza kujiunga na Simba kwa wakati huu kutokana masilahi anayopata Dilian kwenye mkataba mpya ni makubwa kuliko ya Simba.