Mapacha Singida Black Stars, Singida FG sare kila kitu

Muktasari:

  • Sare hiyo ni ya pili mfululizo kwa Ihefu baada ya kufungana pia bao 1-1 dhidi ya Simba huku kiujumla ikiwa ni mchezo wa nne mfululizo kwao katika Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC bao 1-0, Machi 5, mwaka huu.

LIGI Kuu Bara imeendelea tena leo kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo wenyeji Ihefu (Singida Black Stars) wameshindwa katamba kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 ma ndugu zao Singida Fountain Gate katika dabi yao mpya.

Matokeo hayo yamezifanya timu hizo zilingane takribani kila kitu katika msimamo, isipokuwa mabao ya kufunga tu. Timu zote zimecheza mechi 23 kila moja, zimeshinda mechi 6 kila moja, sare 7 kila moja, zimefungwa mabao 31 kila moja na zina pointi 25 kila. Tofauti yao ni Singida FG imefunga mabao 22 wakati Singida Black Stars (Ihefu) imefunga mabao 20 na hivyo Singida FG iko juu ya Singida Black Stars katika nafasi ya 10 na 11 mtawalia.

Katika mchezo huo wa mzunguko wa 23 kwa timu hizo, Singida ilitangulia kupata bao kupitia kwa nyota wa kikosi hicho raia wa Ghana, Nicholas Gyan ambaye shuti la straika wao Elvis Rupia lililokuwa likienda nje lilimgonga nyota huyo wa zamani wa Simba ambaye alikuwa akijaribu kuukwepa mpira ambao badala yake ukatumbukia wavuni katika dakika ya 20 kisha wenyeji Ihefu wakasawazisha katika dakika ya 70 lililofungwa na Joseph Mahundi.

Sare hiyo ni ya pili mfululizo kwa Ihefu baada ya kufungana pia bao 1-1 dhidi ya Simba huku kiujumla ikiwa ni mchezo wa nne mfululizo kwao katika Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga KMC bao 1-0, Machi 5, mwaka huu.

Singida FC imeendeleza matokeo mabaya kwani katika michezo 12 ya Ligi Kuu Bara iliyocheza mfululizo imeshinda mmoja tu, sare minne na kupoteza saba ikiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo baada ya kukusanya jumla ya pointi 25 pia.