Mashabiki sasa hawamtaki Amorim United
Muktasari:
- Hata Man United ilipoonekana kurudi mchezoni, shukrani kwa bao safi la Bryan Mbeumo na kile kichwa cha Maguire, mashabiki wa timu hiyo walipata sababu nyingine muhimu ya kumchukia kocha wao.
Manchester, England. Ruben Amorim amewatibua mashabiki wa Manchester United na hivyo wanataka mabosi wa timu hiyo kumfuta kazi baada ya aibu ya kutupwa nje kwenye Kombe la Ligi na timu ndogo ya Grimsby.
Man United ilipambana kutokea nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya timu hiyo ya League Two na kulazimisha mchezo huo kuingia kwenye hatua ya kupigiana penalti, iliyopigwa kwa dakika 18, Grimsby ikishinda mikwaju 12-11.
Kikosi hicho cha kocha Amorim kilikuwa ovyo kwa muda wote kwenye mchezo na hata beki wa kati, Harry Maguire alipofunga kwa kichwa kwenye dakika za mwisho hilo halikuwafanya kuonekana bora uwanjani.
Ukiweka kando kiwango cha ovyo kilichoonyeshwa na wachezaji wa Man United uwanjani, matendo ya kocha Amorim kwenye benchi lake ndilo lililowafanya mashabiki wa timu hiyo kuamini kocha huyo hana jipya.
Kocha huyo Mreno ambaye yupo kwenye presha kubwa baada ya kichapo kingine kwa timu yake, kwanza alionekana kwenye benchi lake akitazama mafaili yake ya kiufundi kujaribu kubadili hali ya mambo wakati huo timu ikiwa nyuma 2-0.
Kamera za uwanjani zilimnasa Amorim akiperuzi mafaili yake ya kimbinu kuona afanye nini wakati wachezaji wake wakionekana ovyo kabisa uwanjani. Jambo hilo liliwaibua mashabiki wenye hasira wa timu hiyo.
Shabiki mmoja aliandika mtandaoni: "Alipaswa kufukuzwa kazi kabla ya basi la timu halijaondoka uwanjani. Hasameheki."
Shabiki wa pili kwa hasira alisema: "Analeta utoto kwenye mechi!"
Na shabiki wa tatu alisema Amorim alikuwa "anatudanganya tuone yupo bize."
Hata Man United ilipoonekana kurudi mchezoni, shukrani kwa bao safi la Bryan Mbeumo na kile kichwa cha Maguire, mashabiki wa timu hiyo walipata sababu nyingine muhimu ya kumchukia kocha wao.
Wakati wa tukio la kupigiana penalti, mashabiki walimwona Amorim "akijificha" kwenye benchi lake akijizuia kutazama mikwaju hiyo ya penalti iliyopigwa kwa dakika 18. Na shabiki mmoja alisema: "Samahani, lakini sitaki kuwa na kocha ambaye anaogopa kuangalia mikwaju ya penalti dhidi ya timu ya League Two. Hebu rekebisheni hii au fukuza kabisa."
Mwingine alisema: "Amorim alijificha wakati penalti zinapigwa dhidi ya timu ya daraja la nne, hii ni aibu."
Shabiki wa tatu alisema: "Kocha ambaye hata haangalii timu yake dhidi ya mpinzani wa League Two. Hebu toeni huyu Ruben Amorim kwenye klabu yetu."
Na shabiki wa nne alisema: "Amorim akusanye tu mabegi yake. Ameshindwa hata kuangalia penalti, muoga mkubwa."
Kwa matokeo hayo, Amorim amekuwa kwenye presha kubwa kwelikweli ya kuhusu usalama wa kibarua chake huko Old Trafford. Kwa namna hiyo, kocha huyo atalazimika kuomba kwa kila namna kuhakikisha Man United inapata matokeo ya ushindi kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Burnley, Jumamosi huko uwanjani Old Trafford.
Ameshinda mechi moja tu kati ya saba za mwisho alizocheza kwenye michuano yote na sasa akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 37 tu tangu alipotua Man United. Na baada ya mechi hiyo ya Grimsby, Amorim alisema wachezaji kwenye kikos chake hawakucheza kwa ajili yake.
Alisema: "Mwisho wa yote, haijalishi kama tutarudi vizuri au la, unaona dalili zote wakati wa mchezo, hasa mwanzoni mwa mechi. Nadhani timu bora imeshinda, timu pekee iliyokuwa uwanjani.
"Wachezaji bora wamepoteza kwa sababu timu moja inaweza kushinda dhidi ya kundi lolote la wachezaji na nadhani timu ilionyesha hilo uwanjani. Tumepoteza, timu bora imeshinda."
Wacheza kamari wameanza kuwahusisha makocha wengine na kibarua hicho cha Man United wakiamini Amorim hatoboi Novemba kabla hajafungashiwa virago vyake na kuonyeshwa mlango wa kutokea kwenye kikosi hicho.
Makocha waliotajwa ni Gareth Southgate, Michael Carrick, Oliver Glasner, Mauricio Pochettino, Kieran McKenna, Zinedine Zidane, Marco Silva 12, Andoni Iraola, Xavi Hernandez, Simone Inzaghi, Roberto De Zerbi, Diego Simeone, Antonio Conte, Nuno Espirito Santo na Brendan Rodgers.
Mechi za United zijazo
-Agosti 30 vs Burnley (nyumbani)
-Septemba 14 vs Man City (ugenini)
-Septemba 20 vs Chelsea (nyumbani)
-Septemba 27 vs Brentford (ugenini)
-Oktoba 4 vs Sunderland (nyumbani)
-Oktoba 19 vs Liverpool (ugenini)
-Oktoba 25 vs Brighton (nyumbani)