Mashabiki Simba, Yanga wachezea virungu

Kigoma. Mashabiki wa timu za simba na Yanga waliofika katika viwanja vya Lake Tanganyika mjini Kigoma, kuangalia mtanange wa fainali ya kombe la Azam Shirikisho (ASFC), wamelalamikia utaratibu mbovu wa kuingia uwanjani huku wakipigiwa virungu wakiwa katika foleni.

Wakizungumza leo Julai 25, wakiwa katika foleni ya kuingia ndani wamesema utaratibu wa kuwa na kadi na kuanza kuhakiki mmoja mtu mmoja inachukua muda mrefu na kusababisha foleni.

Rajab Said shabiki wa Yanga amesema wangetumia utaratibu wa tiketi za karatasi kama walivyozoea lakini utaratibu huu ni mbovu na kusababisha kupigwa virungu na askari bila sababu.

" Nipo hapa toka saa kumi alfajiri na nimekuwa wakwanza kwenye mstari na hadi wakati huu saa sita mchana sijaingia ndani lakini tunaambulia kupigwa tu,fedha zetu tulipi alafu na kupigwa tupigwe,"amesema Said.

Shabiki wa Simba Jumaa Njombezi, amesema huu utaratibu waliopanga inasababisha watu kukaa juani toka asubuhi watu wapo kwenye foleni wanasubiria kuingia uwanjani.

"Wakati askari na wagambo wanatupiga kuna mtu mmoja shabiki wa Yanga amevunjika mguu wakati wa kusukumana wamepeleka hospitali kupatiwa matibabu, huku wengine wakipoteza vitu vyao kama simu za mkononi, tiketi,pesa na viatu," amesema Njombezi.