Mastaa Man United hawamuelewi Amorim
Muktasari:
- Mabosi wa United bado wanampa sapoti kocha huyo licha ya matokeo ya kichapo katika mechi ya mahasimu wao Manchester City.
Manchester, England. Licha ya wamiliki wa United kudai bado wana imani naye, sauti za wakongwe wa Old Trafford zinasema vingine. Scholes, Neville, Rooney na Keane wameungana kumwaga mzigo mzito kwa Amorim, wakimshutumu kwa kukwama na mfumo wake na kushindwa kuisogeza timu mbele.
Kinara wa mabao wa Man United, Wayne Rooney amefichua kwamba alitazama mechi ya Manchester derby akiwa sambamba na wachezaji wenzake wa zamani.
Kwenye orodha hiyo ya mastaa hao wa zamani wa Man United hakuna hata mmoja aliyekuwa anaelewa Man United inacheza kitu gani uwanjani, huku Rooney akisisitiza hali ya timu hiyo inazidi kuwa mbaya chini ya Amorim.
Baadhi wa mastaa waliopo kwenye kikosi hicho kwa sasa nao wameweka mashaka makubwa katika mtindo huo wa kiuchezaji wa kocha wao, licha ya kwamba bodi bado haijamwambia kuhusu suala la kubadilika.
Rooney amesema kwamba: “Wote tumeona, wote tulikuwa tunapata shida kuona ni kitu gani Man United inacheza. Mfumo ni upi? Kila mtu alishindwa kupata majibu, wote tulicheza soka kwenye kiwango kikubwa sana, hivyo tulikuwa kwenye wakati mgumu kuona kilichokuwa kinaendelea. Sidhani kama kuna yeyote anayeelewa na kukiamini kinachoendelea.
“Baada ya mwaka jana wakati Erik ten Hag alipofukuzwa na kuletwa Ruben, tulisikia timu itakavyocheza na kwamba mambo yatabadilika. Nadhani kama kocha akitaka ukweli wa moyo wake, mambo yamekuwa mabaya zaidi.”
Mfumo mgumu na usiobadilika
Amorim amekuwa akilazimisha mfumo wa 3-4-2-1 bila kujali mpinzani. Scholes amesema wapinzani wanajua wazi namna United wanavyokuja kila wiki: “Ni rahisi kuwadhibiti. Hakuna mabadiliko yoyote. Hakuna ubunifu.” Amesema Paul Scholes.
Ukosefu wa mapambano
“Hakukuwa na mtu wa kusema, ‘hapana, siwezi kukubali.’ Hakukuwa na faulo kali, hakuna kupambana. Wamekuwa laini na dhaifu,” amesema Roy Keane huku akimtaja kipa Bayindir kwa udogo na upole wake.
Uchaguzi wa kikosi
“Fernandes, injini ya kikosi, ameshushwa hadi kucheza kiungo wa chini na kupungukiwa nafasi ya kuunda mashambulizi. Mainoo naye anakosa nafasi huku Maguire akikalia benchi licha ya kuhitajika kwa uongozi wake. Harry Maguire lazima aanze, timu haina kiongozi uwanjani,” amesema Rio Ferdinand.
Kukosekana kwa maendeleo
Miaka 12 baada ya Ferguson kuondoka, hali inazidi kudidimia. Gary Neville amesema: “Kila mmoja anataka kuwa na matumaini, lakini kwa sasa hakuna alama ya maendeleo. Hali ni mbaya zaidi kuliko chini ya Ten Hag.”
Hali ilivyo sasa
Mashabiki wengi waliondoka mapema Etihad, wakionesha wazi kuchoshwa na timu yao. Mechi ijayo ni dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Old Trafford, kisha Brentford na Sunderland kabla ya mtihani mkubwa Anfield dhidi ya Liverpool.
Mabosi wa Man United bado wanampa sapoti kocha huyo licha ya matokeo ya kichapo katika mechi ya mahasimu dhidi ya Manchester City.
Inaelezwa kwamba baadhi ya mastaa kwenye kikosi hicho hawafurahishwi na mtindo wa kucheza na mabeki wa kati watatu, mfumo ambao kocha huyo amekuwa akisisitiza utumike.
Man United ilikumbana na kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Man City chama la Pep Guardiola uwanjani Etihad, hivyo kuifanya kuwa na pointi nne tu katika mechi nne za Ligi Kuu England. Na huo ni mwanzo wa hovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka 1992.
Amorim baada ya mechi hiyo alisema kwamba hatabadili staili yake ya uchezaji ya kumtumia fomesheni ya 3-4-2-1 licha ya kwamba haionekani kufanya vizuri Man United.
Aliongeza kwamba mabosi wa Man United watakachofanya ni kumwondoa kazini kama wataona staili hiyo si njia sahihi ya kuwafikisha kwenye malengo.
Kinachoelezwa ni kwamba mabosi wakubwa wa klabu hiyo ya Man United bado wanampa sapoti Amorim, akimpatia muda wa kutosha kuona kama ataweka mambo sawa.
Mmiliki mwenza, bilionea Sir Jim Ratcliffe alionekana uwanjani Etihad wakati wa mechi hiyo, ambapo picha zilimwonyesha mikono ikiwa kichwani kwa masikitiko ya kile alichokuwa akikiona kwenye mechi hiyo, ambapo Phil Foden na Erling Haaland walitikisa nyavu.
Tajiri Ratcliffe aliifungua pochi kumpa Amorim pesa ya kusajili mastaa wapya, ambapo kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi miamba hiyo ilitumia Pauni 220 milioni kunasa mastaa.
Hivyo, kumfuta kazi kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ina maana kutahitajika kufanya maboresho mengine kwenye kikosi.
Amorim amevuna pointi 31 tu katika mechi 31 alizoingoza Man United tangu alipotua Old Trafford katikati ya Novemba, amepoteza mechi 16 kati ya hizohuku ikichapwa kwenye fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham Hotspur, hivyo haipo kwenye michuano yoyote ya Ulaya msimu huu, ikiwa ni mara ya pili tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013.
United wapo nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu baada ya mechi tano tu, huku wakiwa tayari wameshaondolewa kwenye Kombe la Carabao kwa mikwaju ya penalti na timu ya daraja la nne, Grimsby Town. Hali hii inazidisha ukakasi baada ya msimu uliopita kumaliza nafasi ya 15 matokeo mabaya zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Kocha Amorim mwenyewe anafahamu wazi presha kwa upande wake itazidi kupanda kama matokeo mazuri hayatapatikana, aliposema: “Hii si rekodi inayotakiwa hapa Man United.”
Man United inakabiliwa na mechi ngumu Jumamosi, ambapo itakabiliana na mabingwa wa dunia, Chelsea kipute kitakachopigwa huko Old Trafford. Taarifa ya klabu ilikanusha taarifa za wachezaji wa timu hiyo kupoteza imani na kocha Amorim na kwamba kinachoaminika ni kwamba kocha huyo bado anapewa sapoti na wachezaji wake kwenye vyumba vya kubadilishia.